Ticker

6/recent/ticker-posts

SIMBA SC YATINGA NUSU FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA KWA KISHINDO

 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Klabu ya Simba SC imeendeleza rekodi yake ya kutisha kwenye michuano ya kimataifa baada ya kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), kwa ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Al Masry ya Misri. 

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, umemalizika kwa dakika 90 za kawaida kwa Simba kushinda mabao 2-0, hali iliyofanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 baada ya Al Masry kushinda kwa idadi hiyo hiyo kwenye mchezo wa kwanza.

Mabao ya Simba yamefungwa na Elie Mpanzu pamoja na mshambuliaji matata Steven Mukwala.

 Hatua ya penalti ikaamua hatma ya mchezo, ambapo walinda mlango na wapigaji wa Simba walionesha utulivu na umahiri wa hali ya juu, na hatimaye kutinga Nusu Fainali kwa kishindo.

Katika hatua inayofuata, Simba SC itakutana na mshindi kati ya Zamalek ya Misri dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini – mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka ndani na nje ya Tanzania.

Kufuatia ushindi huo wa kihistoria, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za pongezi kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa Simba.

 Kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Rais Samia ameandika:

“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup). Ushindi wenu ni furaha kwa mashabiki wenu na burudani kwa Watanzania wote. Ninawatakia kila la kheri katika Nusu Fainali.” – Rais Samia.

Simba sasa inabeba matumaini ya taifa katika kulinda heshima ya Tanzania kwenye anga za soka la Afrika, huku mashabiki wakingoja kwa shauku kuona historia ikiandikwa.






Post a Comment

0 Comments