Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 17, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 17, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
**
Katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali kupitia Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imewekeza sh bilioni 25.7, kwa ajili ya kufanya utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia katika maeneo mbalimbali.
Aidha katika uongozi wake huo, kuanzia (2021-2025)Tanzania inaendelea kupiga hatua katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa utashi thabiti wa kisiasa na dira ya kulifanya taifa linalojengwa kwa kutumia sayansi na teknologia.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu jijini Dodoma wakati akitaja mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan toka aingie madarakani.
Amesema hatua hii si tu kwamba imeendelea kuimarisha msingi wa maendeleo ya kisayansi, bali pia imethibitisha dhamira ya Serikali ya kujenga taifa linalowekeza katika kuibua teknolojia, likiongozwa na tafiti na ubunifu.
Dkt. Nungu amesema Serikali kupitia COSTECH, imefadhili zaidi ya tafiti 50 katika sekta za Elimu, kilimo, afya, na mazingira ili kuhakikisha maarifa haya yanatumika kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesema mpaka sasa zaidi ya vituo vya ubunifu 111 vimeimarishwa, huku tafiti zikibadilika kuwa suluhisho kisayansi kwa jamii, zikiwemo kampuni mpya zipatazo 70 zimesajiliwa yote hayo yakiwa na matokea ya wabunifu waliyowezeshwa na Serikali.
Dkt. Nungu amesisitiza kuwa, Serikali ya awamu sita imetoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa kitanzania ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyokusudia.
Amesema kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu.
Amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku shilingi milioni 600 zikielekezwa katika miradi minne ya usalama wa chakula, ikihusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao, uboreshaji wa uhifadhi wa chakula na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu.
0 Comments