BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeandaa kuadhimisha Siku ya Kuondoa taka (International day of zero waste) ambayo yatafanyika Machi 28 hadi 30, 2025 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam
Akizungumza Machi 22,2025 katika IFTAR iliyoandaliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mhandisi Hamad Masauni na NEMC, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Semesi amesema maadhimisho hayo ni mahususi kwa kuyaleta pamoja makundi mbalimbali ya wadau wa mazingira kwa lengo la kuangazia umuhimu wa usimamizi endelevu wa taka na kukuza uchumi mzunguko (promote a circular economy).
"Hii itakuwa ni fursa nyingine nzuri kwetu sote kukutana tena na kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu katika kutafuta masuluhisho ya pamoja ya changamoto za kimazingira zinazotukabili". Amesema
Amesema kuwa licha ya mafanikio mengi yaliyofikiwa katika usimamizi wa mazingira, bado kuna mambo mengi yanahitajika kufanywa ili kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika ngazi zote, kushirikisha jamii, kuongeza uelewa, kubuni njia mbadala za kujikimu kama wahusika wakuu wa kusaidia kuzuia na kukabiliana na athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu (anthropogenic activities) zinazosababisha uharibifu wa mazingira, athari kwa rasilimali za maji na hatimaye changamoto za maisha.
Pamoja na hayo Dkt. Semesi amesema kazi inayofanywa na wadau mbalimbali katika kuhifadhi, kulinda na kusimamia mazingira inafaida kubwa kwa mazingira yetu katika kutimiza maandiko ya vitabu vitakatifu.
Amesema amesema Dini ina mchango mkubwa katika kutunza na kuhifadhi Mazingira kwani vitabu vya Dini vimeeleza na kutoa vifungu vinavyoeleza juu ya utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira.
"Sote tunajua Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili na mifumo ikolojia ya kipekee ambayo ni pamoja na aina nyingi za mimea, wanyama, wadudu na ndege. Kwa pamoja tunatakiwa kuhakikisha tunapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira kama vile uchimbaji madini, ufugaji na kilimo visivyo endelevu na kuepuka ukataji mkubwa wa misitu." Ameeleza Dkt. Semesi.
0 Comments