Na Mwandishi Wetu, KIGOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ameongoza jopo la wataalamu wa msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kutoa huduma na elimu ya uraia kwa wananchi wa Kata ya Kibirizi iliyopo Manispaa ya Kigoma, mkoani Kigoma.
Dk.Ndumbaro ambaye yupo mkoani humo jana walipiga kambi kwenye Kata hiyo na kusikiliza na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu changamoto za masuala ya kisheria.
Katika kampeni hiyo ambayo imeanza juzi mkoani humo na inalenga kuvifikia vijiji 240 mkoani humo, Waziri Ndumbaro alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza wananchi wapewe elimu hiyo sambamba na elimu ya sheria na Katiba, Haki za binadamu na msaada wa kisheria ili wajue sheria na kupata haki zao.
“Tanzania ni nchi nzuri yenye kuvutia wema na wabaya, yenye neema kedekede sisi tumejaa neema, ina amani na utulivu na mfumo mzuri wa maisha, kuna nchi hazina haya tuliyo nayo sisi, uzuri huu unawavutia wengi wengine wanakuja kwa kufuata taratibu rasmi za uhamiaji, wapo wanaokuja kwa njia za panya hawa ndio wanaotuponza,”alisema.
Alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuwa makini kwa kuwa tatizo la mipakani kuna kuingiliana kwa makabila na nchi jirani.
“Tusiwapokee watu kwasababu tuna share nao makabila, juzi tulikuwa na kesi moja kuna raia wa Burundi walikaa huku wakapewa uraia, mmoja aliyepewa uraia ameenda Burundi anaongoza chama cha siasa, huku tunamjua kama mtanzania lakini nchi Jirani anaongoza chama cha siasa hiyo ni sawa? Hapa ndipo mgogoro unapokuja,”alisema.
Alisema katika kampeni hiyo Kigoma watatoa elimu ya uraia kwa kuwa masuala ya uraia ni magumu hasa maeneo ya mipakani.
“Lazima tufahamu sheria, suala si kuzaliwa tu endapo ulizaliwa na mmoja wa wazazi sio mtanzania unapaswa ufanye nini kwa mujibu wa sheria, unakwenda uhamiaji unasema Baba yangu alikuwa Mrundi na mama yangu Mtanzania nimefikisha umri wa miaka 18 nachagua sasa kuwa Mtanzania naomba mnihalalishe,”alisema.
Alifafanua kuwa gharama za huduma za kisheria ni kubwa ndio sababu iliyomsukuma Rais Samia kubuni kampeni hiyo ili kuwasogezea wananchi huduma za kisheria popote walipo.
“Wataalamu hawa wapo kwenye Kata 80 na Vijiji 240 wanaendelea kusikiliza na kutatua kero za kisheria za wananchi wa Kigoma, huyu ni Rais mwenye uchungu na wananchi wake wanyonge, Mama huyu tuna kila sababu ya kusimama naye hasa mwaka huu 2025,”alisema.
Alieleza kuwa kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza mwisho wake ni mwakani 2026 na ili kufanikisha ni muhimu wananchi kumchagua Rais Samia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili aendelee kuwasogezea huduma za kisheria.
Awali, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda alisema ni maono ya Rais Samia wananchi wapate nafasi ya kusikilizwa na wapewe msaada wa kisheria kwenye changamoto zao.
“Wananchi hawa wana kadhia nyingi zinazotokana na mambo ya sheria kuhusu hukumu zinazotolewa na Mahakama, nakala za hukumu, namna ya kusikiliza mashtaka, upelelezi, kukaa muda mrefu rumande, umiliki wa viwanja,”alisema.
Alisema pamoja na matatizo mengine ya kisheria yaliyopo Kigoma Mjini kuna suala la utata wa uraia wa watu.
“Kuna watu mababu zao wamezaliwa Kigoma na wamefia Kigoma, msaada wa kisheria namba moja tunaohitaji ni kutatua utata wa uraia wa watu, watu wameomba namba za NIDA hawajapata, watu wamepeleka hadi wazazi wao lakini bado wameonesha na makaburi ya wazazi wao lakini bado wanapata misukosuko,”alisema.
Alisema kuna tatizo la watu kuhusisha kabila na Taifa na kwamba msaada huo wa kisheria utatoa tabasamu kwa wananchi ambao wamekosa watu wa kuwatetea kwenye changamoto zao za kisheria.
0 Comments