Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZEE WAISHUKURU SERIKALI KWA KUBORESHA USTAWI WAO


Na WMJJWM-Dodoma

Wazee nchini wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma muhimu kwa Ustawi wa Wazee ikiwemo huduma za Afya, Msaada wa Kisaikolijia na kuboresha Miundombinu ya Makazi ya Wazee wenye changamoto nchini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa Lameck Sendo Januari 20, 2025 alipokutana na kuzungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ofisini kwake jijini Dodoma.

Aidha, Mzee Sendo ameipongeza Wizara kwa kuratibu vyema mchakato wa Mapitio ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 toleo la 2023 ambayo ipo katika hatua za mwisho ili iweze kuanza kutumika na baadae kuwezesha mchakato wa utungwaji wa Sheria ya Wazee nchini.

“Kwa kweli Wizara inafanya kazi kubwa kwenye eneo la kuimarisha Ustawi wa Wazee na ni imani yetu kwamba Serikali hii itaendelea kuwatambua Wazee na kuwapatia Huduma Bora za Afya ikiwemo Bima na kuwashirikisha katika masuala yanayowahusu kama vile uchumi, siasa, familia na Jamii kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho" amesema Mzee Sendo

Pia Mzee Sendo ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao na kuwashirikisha katika kutoa maoni kwenye mchakato wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema Serikali ya Awamu sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhakikisha wazee wanapata huduma bora katika maeneo yao pia na wale waliopo katika makazi ya wazee ikiwemo matibabu, lishe na ulinzi.

Aidha Dkt. Jingu amesema katika kuboresha zaidi ustawi wa Wazee nchini, Serikali itaendelea kupokea maoni na ushauri wa Wazee juu ya namna njema ya kuboresha Huduma na Ustawi wa wao kwa ujumla.

Dkt. Jingu ametoa wito kwa Jamii kuendelea kuwalinda Wazee, kwani wao ni Tunu muhimu na kutumia maarifa waliyonayo katika masuala mbalimbali ikiwemo malezi na Makuzi ya Watoto, kupambana na vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili.

Post a Comment

0 Comments