Kampuni ya Dhahabu ya Barrick imeingiza zaidi ya dola bilioni 4.24 katika uchumi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwa ubia wa Twiga kati yake na Serikali ya Tanzania mwaka 2019, na kuchangia dola milioni 888 katika mwaka 2024 pekee.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, Januari 23, 2025, Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema kuwa ubia wa Twiga unaohusisha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu umeendelea kuwa kiongozi katika tasnia ya uchimbaji madini nchini Tanzania, ukichangia kwa maelfu ya ajira, kusaidia biashara za ndani na kufadhili miradi muhimu ya kijamii.
"Tulitumia dola milioni 573 kwa wasambazaji na watoa huduma wa ndani mwaka jana, sawa na asilimia 83 ya matumizi yetu yote. Aidha, 75% ya malipo yetu yote kwa watoa huduma na wasambazaji yalikwenda kwa makampuni ya wazawa, yakivuka lengo letu la 61%," amesema Bristow.
Ameongeza kuwa kutokana na sera ya Barrick ya kuendeleza ajira na maendeleo ya ndani, 96% ya wafanyakazi wa Barrick nchini Tanzania, wapatao 6,185, ni Watanzania, huku 53% wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi.
"Mnamo mwaka huo huo, Barrick iliwekeza zaidi ya dola milioni 5 katika miradi ya maji safi ya kunywa, huduma za afya, na elimu, na kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi ya kijamii kufikia dola milioni 15.8 tangu Barrick ichukue jukumu la uendeshaji wa migodi ya Tanzania mwaka 2019," amesema.
Migodi ya Bulyanhulu na North Mara ilifanya vizuri katika utekelezaji wa uzalishaji wa mwaka 2024, ikidumisha hadhi yao kama rasilimali za kimkakati zenye uwezo wa kuwa "Daraja la Kwanza."
Pamoja na hayo, amesema migodi hiyo miwili iliendelea kuzingatia usalama wa hali ya juu, ikitimiza mwaka mzima bila matukio yoyote ya majeraha makubwa yaliyoweza kupunguza muda wa kazi.
Kwa upande wa mgodi wa Buzwagi, mgodi huo ulifanya maendeleo makubwa katika utekelezaji wa ufungwaji wake, huku ukizingatia usimamizi wa mazingira, hasa kuhusu maji na utunzaji wa uoto wa mimea.
Amefafanua kuwa, Ukanda Maalum wa Kiuchumi ulioanzishwa katika eneo hilo umefikia hatua za juu za maendeleo, huku ukiwavutia wawekezaji. Kampuni moja tayari imesajiliwa katika Ukanda wa Uchakataji wa Bidhaa za Kuuzwa Nje ya Nchi.
Kuhusu Chuo cha Barrick Buzwagi kilichofunguliwa mwaka 2024 amesema kimefanya maendeleo makubwa katika kukuza vipaji vya Barrick.
"Kikiwa kimejikita katika utoaji mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu, chuo hicho tayari kimetoa mafunzo kwa watu wapatao 1,700 na kinatarajiwa kuvuka lengo lake la kutoa mafunzo kwa zaidi ya watu 2,800 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025",ameeleza.
Aidha ,Uchimbaji rejeshi katika migodi ya North Mara na Bulyanhulu umefanikisha kurejesha mali ghafi zinazochakatwa ili kupata dhahabu.
"Barrick inaendelea pia kuimarisha juhudi zake za utafutaji madini katika Wilaya ya Nzega, eneo linalotarajiwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini. Hii itachangia zaidi ya kilomita za mraba 2,000 za maeneo mapya yatakayosaidia katika ukuaji wa hifadhi ya madini kwa ajili ya migodi ya North Mara na Bulyanhulu",amesema Bristow.
Upanuzi huu ni sehemu muhimu ya mkakati wa muda mrefu wa Barrick wa kutambua na kuendeleza maeneo yenye uwezo wa kuzalisha migodi mingine yenye hadhi ya "Daraja la Kwanza" katika ukanda huu.
"Twiga ilipata sifa nyingi katika mwaka uliopita, ikiwa ni pamoja na kutambuliwa kwa usalama wake, mwajiri bora, utendaji wa kimazingira, na ushirikishwaji wa jamii. Mnamo mwaka 2024, mgodi wa North Mara ulitambuliwa kama mchangiaji mkubwa zaidi wa uchumi katika tasnia ya uchimbaji madini nchini Tanzania",ameeleza Bristow.
Migodi yote miwili ilipokea tuzo kadhaa kutokana na dhamira yake ya kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi, uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, na uzingatiaji wa utaratibu wa kutumia malighafi na rasilimali za ndani.
"Kazi ya Barrick nchini Tanzania ni kielelezo cha uchimbaji madini endelevu unaoweka uwiano baina ya uwajibikaji wa kiuchumi, kimazingira, na kijamii," amesema Bristow.
"Kutambuliwa kwetu tulikokufikia ni ushahidi tosha wa dhamira yetu katika kuhakikisha ubora na thamani tunayoiletea Tanzania",ameongeza.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini na kufanya usimamizi madhubuti ili kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha pande zote.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ameipongeza Barrick kwa uwekezaji wake mkoani humo, ambao unaendelea kuchangia pato la Serikali sambamba na kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii, huku akifafanua kuwa mgodi wa Buzwagi umefungwa kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Iddi Kassim, ameeleza kuwa wananchi wa Msalala wanaendelea kushirikiana na Barrick katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, afya, na miundombinu ya barabara.
Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari
0 Comments