Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAPONGEZWA KUWA KINARA WA MASUALA YA AMANI NA USALAMA UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kuwa kinara katika masuala mbalimbali yanayolenga kuleta amani na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam leo tarehe 17 Januari 2025, jijini Dodoma, ambapo yupo katika ziara ya kikazi.

Akiwa jijini Dodoma Bw. Borgstam kwa nyakati tofauti amefanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) ambaye alimwakilisha Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) na Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambayo yalikita kujadili kuhusu masuala ya ulinzi na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Katika mazungumzo na viongozi hao Bw. Borgastam ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya unatambua na kuthamini mchango wa kipekee unaotolewa na Tanzania katika kuleta amani na usalama wa kudumu katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu zinazokabiliwa na changamoto za kisiasa ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Bw. Borgastan aliongeza kusema kuwa ziara yake hapa nchini inalenga kupata na kubadishana uzoefu na Tanzania kuhusu masuala ya usalama na amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, kwa kuwa daima Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuendesha operasheni mbalimbali na majadiliano ya kuleta ufumbuzi wa kudumu juu ya changamoto za kisiasa zinazokabili Ukanda huo.

Aidha, aliendelea kusema kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Tanzania katika kuleta amani na usalama Ukanda wa Maziwa Makuu.

Kwa upande wao Viongozi wa Tanzania, wameushukuru Umoja wa Ulaya kwa mchango wake wa aina mbalimbali wanaoendelea kutoa katika kuhakikisha Ukanda wa Maziwa Makuu unakuwa na amani ya kudumu ili wanachi wake wawe huru kuendesha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa mustakabali mwema wa kizazi cha sasa na kijao.

Ukanda wa Maziwa Makuu una jumla ya Nchi Wanachama 12, ambao ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam yaliyofanyika jijini Dodoma. 
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) katika picha ya pamoja na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma. 
 Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma. 

Post a Comment

0 Comments