Ticker

6/recent/ticker-posts

SALAMU ZANGU ZA MWAKA 2025 KWA RAIS DK.SAMIA NA CCM YAKE


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

Mimi Said Mwishehe kwanza kabisa kwa kipekee naomba nimshukuru Muumba wa mbingu na ardhi kwa kutujaalia afya na uzima na leo tuko mwaka 2025, Tumevuka mwaka salama kwa uwezo wake maanani.

Tunafahamu mwaka 2024 ulikuwa mwaka wenye mafanikio na changamoto zake lakini tumevuka na sasa tunaaanza safari ya mwaka 2025.Tumuombe Mungu atuweke, atupe afya njema na uhai tuumalize mwaka 2025, Tuseme Inshallah.

Baada ya utangulizi huo wa salamu naomba pia niendelee kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kuendelea kuwa wamoja na kuhakikisha tunasimamia misingi iliyowekekwa na waasisi wa taifa hili na hasa suala la zima la kutunza amani ya Nchi yetu .

Pia najua mwaka 2024 ulikuwa ni mwaka wa kufosi na kuna Msanii mmoja wa bongo Fleva katika sehemu yake ya Mashairi mbali ya kusema huu ni mwaka wa kufosi akaenda mbali zaidi kwamba lazıma watamuita bosi, hivyo ni wakati wa kutafakari kuwa tumefosi na kuitwa bosi au tumekwama?Tujipange mwaka 2025 naamini kila kitu kitakaa sawa, acha uoga.

Naomba nirejee katika hoja yangu ya msingi ambayo inanifanya niandike salamu zangu za mwaka 2025 kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na Chama Cha Mapinduzi(CCM) ambacho wewe ni Mwenyekiti wake Taifa.

Rais wangu Dk.Samia Suluhu Hassan, Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya salamu hiyo na baada ya kujibu Kazi Iendelee naomba niseme mapema kabla ya kukuchosha, Naomba nikupongeze kwa kazi kubwa na nzuri unayoendelea kuifanya ya kuwatumikia Watanzania.

Tangu umekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeonesha uzalendo mkubwa katika kulitumikia Taifa la Tanzania,umekuwa Rais mwenye upendo,huruma kwa wananchi unawaongoza na kubwa zaidi umekuwa msikivu,hongera Rais Samia.

Uongozi wako umekuwa ukitanguliza zaidi hekima na busara katika kufanya maamuzi yako kwa ajili ya nchi yetu,hakika uongozi wako unaifanya Tanzania kuwa katika mikono salama,hakika tunajivunia uongozi wako.Dk.Samia wewe ni Rais, wewe ni Mama yetu.Upendo wako unaishi katika mioyo yetu.

Nakumbuka wakati unachukua kijiti cha uongozi kutoka kwa mtangulizi wako Hayati Dk.John Pombe Magufuli, ulituhakikishia Watanzania kuwa nchi iko katika mikono salama.Wenye mashaka na wewe uliwaambia wasiwe na wasiwasi nchi itakwenda,miradi yote itatekelezwa na kukamilika na utaanzisha miradi mingine.

Hakika mimi na Watanzania wenzangu tumeshuhudia kazi kubwa ambayo umeifanya na unayoendelea kuifanya kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.

Rais Samia naomba upokee salamu zangu za kukutakia heri ya mwaka mpya wa 2025.Nakuombea afya njema,nakuombea uendelee kuwa mwenye hekima na busara katika uongozi.Tunajivunia uongozi wako.Nchi imetuliaa hadi raha.

Wakati unachukua Nchi wapo baadhi ya watu walikuwa wanakuchukulia poa, walidiriki kusema hutaweza,hutaweza kutekeleza miradi.Leo hii wale watu wamefunga midomo,waliko wanaona aibu.Kazi kubwa ambayo umeifanya kwa kweli kwa lugha ya watoto wa mwaka 2000 ni kwamba umewanyoosha.Wametulia huko waliko.

Wakiangalia bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere kazi imefanyika na umeme umeunganishwa katika gridi ya Taifa,tumeanza kuonja utamu wa Mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere.Naamini mradi utakapokamilika kwa mitambo yote kufanya kazi kwa asilimia 100 mbona tutajibweda,tutajinoma sana.

Mradi wa reli ya kisasa kwa ajili ya treni ya umeme maarufu kama SGR wote ni mashahidi,kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na Dar es Salaam kwenda Dodoma sasa tunajidai tu. Unalala Dodoma chai unakuja kunywa Dar.

Nakupongeza Rais Samia kwa kusimamia vema Mradi wa reli ya SGR, nafahamu kazi ya Ujenzi kutoka Dodoma kwenda Mwanza na baadae Kigoma kazi inakwenda vizuri sana,unastahili pongezi Rais Samia.Wale ngedere wanaokata umeme na kuharibu miundombinu ya SGR najua chini ya uongozi wako dawa yao iko jikoni.

Najua kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya Rais Samia katika Nchi yetu,miradi ya miundombinu ya barabara imeendelea kuboreshwa chini ya Serikali unayoingoza, kwa Dar es Salaam barabara za mwendo kasi unaendelea kuzijenga na umegusa barabara zote muhimu.

Miradi ya barabara hizo ukikamilika Dar itakuwa tamu mnoo.Najivunia kuwa na Rais Samia.Ujenzi wa miundombinu ya barabara unaifanya katika kila kona ya nchi yetu,Watanzania ni mashahidi.

Hata hivyo Rais Samia wakati natuma salamu hizi za mwaka mpya kwako naomba nikukumbushe wakazi wa Majohe Kwasoma walioko katika Jimbo la Ukonga Jijini Dar es Salaaam tunakuomba barabara ya lami , nafahamu kipande cha urefu wa mita 200 tumewekewa lami na vitaa vya juu.

Kuwekwa lami kwa kipande hicho kidogo sana kunaashiria barabara ya kutoka Sekondari ya Pugu kwenda Majohe Kwasoma,Halisi hadi kwa Mpemba tutapata lami katika mwaka huu wa 2025, ndio kılio chetu kikubwa wakazi wa Majohe Kwasoma.

Ikikupendeza Rais wangu tusaidie lami katika barabara yetu ya Majohe Kwasoma hadi kwa Mpemba kwani utakuwa umetatatua changamoto kubwa ya usafiri halafu kuhusu tunakula na kuvaa nini hilo tuachie wenyewe.

Ngoja tuachane na ombi la barabara ya lami ya Majohe Kwasoma, nijikite katika salamu zangu za mwaka mpya kwako Rais Samia, naomba nikupongeze kwa hatua unazoendelea kuchukua kuboresha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu ya huduma za afya, kununua Dawa na Vifaa Tiba.Umeongeza bajeti ya sekta ya afya.Bohari ya Dawa (MSD) wameendelea kuboresha huduma zao.

Katika afya Rais Samia naomba nikwambie tu kama kuna eneo ambalo binafsi nimefurahishwa ni katika suala la Bima ya Afya kwa wote, katika eneo mojawapo ambalo Watanzania tunapata changamoto ni gharama za matibabu ya afya.

Gharama ziko juu na kwa Mtanzania hasa wa kipato cha chini anashindwa kumudu ndio maana tunaishia kununua Panado tu, uwezo kwenda hospitalini haupo, Nani anaweza gharama zake?

Kwa kuliona hilo Rais wetu mpendwa tumeona hatua ambazo umeendelea kuzichukua zikiwemo za kutoa maelekezo yako kwa Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) kuwa na Bima ya Afya kwa Wote.Tunaona hata mchakato umefika hatua nzuri, tumeanza kuona dalili njema.

Sasa Watanzania tunakwenda kufurahia huduma za afya kupitia bima ya afya kwa wote.Kuhusu bima ya afya kwa watoto Rais umetoa maelekezo yenye busara kwa NHIF na sasa watoto wakiwemo wanafunzi wamerejeshea kifurushi cha Toto Afya Kadi.

Kiiliondolewa hapo katikati na kuwababisha malalamiko lakini Rais umekirudisha na hii inathibitisha upendo wako mkubwa kwa watoto wa Taifa hili.Hongera kwa juhudi zako katika sekta ya afya.Hupendi kusifiwa lakini naomba uniruhusu nikusifu maana unastahili.

Katika eneo la utunzaji mazingira Rais Samia pamoja na hatua mbalimbali ambazo Serikali yako imeendelea kuchukua tunashuhudia mkazo ambao umeuweka katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, sasa ni mwendo wa gesi tu na muda si mrefu mkaa na kuni vinakwenda kubaki kuwa historia.

Wananchi wanatunza mazingira na wakati huo huo wanatunza na afya zao.Nani anapenda kuwa na macho mekundu kwasababu ya moshi wa kuni ?Tunakushukuru Rais Samia na ni matumaini yangu hamasa ya nishati safi itaendelea kuelekea 2032 kama ambavyo umeelekeza.

Rais Samia naomba wakati unasoma salamu hizi utambue kuwa Watanzania tunakupenda, tunajivunia uongozi wako ambao umetufanya tuwe na amani ya moyo, hakuna mwenye presha na watu wanaendelea na shughuli za utafutaji kwa utulivu kabisa.

Hakuna mwenye wasiwasi ,watu wametulia na maisha yanakwenda.Walioko maofisini na hasa watumishi wa Umma wanatekeleza majukumu yao bila ya kuwa na mawazo ya kwamba je itakuaje?Wanaokosea unachukua hatua zinazostahili bila kuonea mtu.Mungu amekujaalia utu,amekujaalia hekima na busara.

Rais Samia umeyafanya mengi na hayo ndio ambayo yanafanya niandike salamu hizi moyo wangu ukiwa na matumaini makubwa na uongozi wako,najua pamoja na mafanikio makubwa ya uongozi wako kama Taifa tumepitia changamoto ya baadhi ya watu kupotea.

Kelele zimekuwa nyingi,familia ambazo zimepotelewa na ndugu ,jamaa na marafiki wamepaza sauti,Watanzania wametoa vilio vyao katika hili. Hata hivyo hili la watu kupotea linahitaji mjadala mpana lakini wenye kutuunganisha zaidi na si kutugawa.

Hata hivyo nikiri nilifurahishwa na maelekezo yako Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanachukua hatua kudhibiti matukio hayo.Umetoa rai kwa Watanzania kutoa ushirikiano katika kukomesha matukio hayo.

Hivyo wakati natoa salamu zangu za mwaka mpya kwako natumai utaendelea kutoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua kuhakikisha matukio ya watu kupotea yanakoma.Hakuna anayefurahishwa na matukio hayo.Uso wa Rais anapozungumzia watu kupotea umekuwa ukionesha anavyoumizwa nayo.Pole Rais wetu.

Katika salamu zangu kwako Rais Samia naomba nikupongeze kwa kazi kubwa ambayo unaendelea kuifanya katika sekta ya kılımo kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo zinahusika na kilimo.Umeondoa kero ya kuchelewa kwa pembejeo za kilimo.Umeweka nguvu katika kutafuta Masoko ya mazao yetu, umeondoa tozo na kodi ambazo zilikuwa kero kwa wakulima.

Rais Samia Samia kwa sasa kilimo kimekuwa kimbilio la Watanzania walio wengi, watu wako mjini wanafunga tai shingoni lakini kijijini wanamashamba ,wanalima,wanavuna na kisha wanapiga Pesa.Rais Samia umekuwa na mtazamo chanya katika kilimo, nafahamu fedha ambazo umeelekeza ziende katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji.

Hakika unastahili pongezi,nikwambie Rais Samia katika kilimo unaupiga mwingi sana ingekuwa mchezaji basi nakufananisha na Awesu Awesu maarufu kepteni Lucho fundi wa boliii.Hapo natania tu kwani wewe ni namba moja kwangu katika kila kitu kinachohusu nchi yangu nzuri.Hongera Rais Samia ,ipo siku nitakuja kukusalimia Live Ikulu maana katika ndoto nilishakutana na wewe na tukazungumza mengi.

Lakini katika sekta ya maji nako tunaona hatua unazoendelea kuchukua kampeni yako ya kumtua ndoo mama kichwani imefanikiwa. Maelekezo yako ya maji yawe yanapatikana ndani ya mita 400 yamefanyiwa kazi.Shida ya maji inaendelea kupungua.

Juzi maelekezo yako baada ya kuona ile video ya mtangazaji wa Clouds TV kule Tanga nayo imenigusa sana, umeona tatizo na umechukua hatua na leo wananchi wale wanakunywa maji safi na salama, yale maji ya machafu waliyokuwa wanakunywa siku zote muda si mrefu watasahau.

Ngoja nirudi katika michezo Rais Samia umeweka nguvu kubwa katika Michezo yote na tumeanza kuona matunda yake , umetuwekea goli la Mama ambalo hakika timu zinavuna hela, huna baya mama, ni jambo la kawaida kuona kuona kapu la fedha uwanjani.Wachezaji wanaogelea fedha tu na juzi umekuja na Knock Out ya Mama,bondia Karim Mandonga amechukua fedha baada ya kumpiga mpinzani wake Said Mbelwa.

Katika Utalii Rais Samia tunaona matunda ya filamu yako ya Royal Tour, Utalii umeendelea kupaa nchini, fedha za kigeni zinazotokana na utalii zimeendelea kuingia nchini. Kuimarisha sekta ya utalii tunashuhudia hata Hadzabe nao wamekuwa kivutio kikubwa baada ya kutangazwa.

Tunafahamu walikuwepo lakini hakuna aliyekuwa akiwafuatilia lakini kupitia wewe leo wamekuwa maarufu na wao wamekuwa kivutio kwa Watalii wanaokuja nchini na wanapiga Pesa.

Hata hivyo baada ya kueleza hayo naomba nikwambie na najua unajua Rais wangu unafahamu

kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila baada ya miaka mitano tunafanya uchaguzi Mkuu kuchagua madiwani,Wabunge na Rais,hivyo mwaka huu wa 2025 Watanzania tutakuwa na uchaguzi Mkuu.

Hivyo ni mwaka wenye mishe mishe nyingi zinazohusu chaguzi,tutasikia mengi,tutaona mengi lakini tumejiandaa nayo.Tunamuomba Mungu atuvushe salama,tufanye uchaguzi uliojaa utulivu na amani.Ni matumaini yangu Mungu yuko pamoja nasi wakati wote.

Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi najua kwa nafasi ya Rais Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakusimamisha wewe Dk.Samia kugombea nafasi hiyo .Sina mashaka na wala Watanzania hatuna shaka yoyote na uwezo wako kwani uliyoyafanya katika uongozi wako umethibitisha uwezo wako, nchi iko salama na maendeleo yamepatikana chini ya uongozi wako.

Kwa uwezo wako Dk.Rais Samia ambaye pia ndio Mwenyekiti wa CCM Taifa sitarajii kuona akitokea mwanaCCM mwingine akichukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais.

Najua kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwana ccm anaweza kuchukua fomu ndani ya Chama lakini kwa utaratibu wa Chama hicho ambao umekuwepo kwa muda mrefu huwa Rais anapokaa kwa awamu ya moja basi huachiwa aendelee na awamu ya pili kukamilisha awamu mbili za Urais ,miaka mitano awamu ya kwanza,miaka mitano mingine awamu ya pili.

Kwa mujibu wa Katiba Rais atakaa miaka 10 kama watanzania wataridhia kupitia sanduka la kura.Ni kweli Rais Samia ulichukua nafasi ya kuwa Rais baada ya kifo cha Dk.John Magufuli lakini kwa mujibu wa utaratibu Rais Samia ndio anayepewa nafasi tena ndani ya Chama hicho ili aendelee kuwaongoza Watanzania.

Hivyo kwa utaratibu huo huo ambao umekuwepo kwa muda mrefu na kuwa sehemu ya utamaduni wa CCM katika salamu zangu kwako Rais Samia nakuomba wakati ukifika chakua fomu ya Urais ndani ya Chama chako na binafsi katika uchaguzi Mkuu tutakapojaaliwa afya na uzima basi kura yangu nikuhakikishie inakusubiria wewe.Nisipokupa wewe nampa nani?

Kwa kazi kubwa na nzuri ambayo umeifanya tangu uingie madarakani Watanzania tumeridhika na uongozi wako na nina uhakika tutakuchagua wewe Rais Samia katika uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Watanzania wanakusubiria kwa hamu na wameonesha dalili za ushindi wako Rais Samia mapema kabisa, tunakumbuka mwaka 2024 nchi yetu imefanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wagombea wa CCM wameshinda kwa asilimia 99 .Ushindi huo wa CCM unathibitisha hamu waliyonayo Watanzania kuwa Rais Samia utashinda katika uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa kishindo.

Niwaombe Wana CCM kuweka nguvu zao katika kukupambabnia Dk.Samia urejee katika kiti cha Urais, sina shaka na uimara wa Chama chako,sina shaka na mipango na mikakati ya CCM linapokuja suala la uchaguzi.Katibu Mkuu Dk.Emmanuel Nchimbi anajua nini cha kufanya.

Hata hivyo najua kwa hulka ya binadamu huwa tunakuwa na matamanio na ndoto zetu na katika siasa wapo wanaotamani kuwania Urais lakini kama kuna wana CCM wanaotaka nafasi hiyo ni vema wakatumia hekima na busara wakakuacha Rais Samia uendelee kututumikia.

Ningeambia niishauri CCM basi ushauri wangu ungekuwa katika uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa ngazi ya Chama fomu ya Mgombea Urais iwe moja kwa ajili ya Dk Samia tu.Kwanza kutoa mafomu mengi kwa nafasi ya Urais ni matumizi mabaya ya rasilimali fedha.

Rais Dk.Samia unatosha na mitano tena ni jambo ambalo halina mjadala,wengine ndani ya CCM wasubiri 2030 kama wanahitaji.Ninaposema hivi wanaoutaka Urais wananiona kama vile nimechanganyiwa,wananiona mimi ‘Chawa’,wananiona Mnoko sana.Wananiona sina uwezo wa kufikiria.Watu bwawa!!!

Niwaambie naeleza haya nikiwa na akili zangu timamu na sijashawishiwa na mtu yeyote, kwanza ni salamu zangu tu kwa Rais wewe unaumia nini? Au ndio unautaka Urais?Kwanza hizo sifa unazo za kupambana na Dk.Samia?Hovyoo.

Mwaka 2025 ni mwaka wa Rais Samia ,iwe jua ,iwe mvua tuko naye.Najua kwa mujibu wa Katiba nchi yetu iko katika Mfumo wa vyama vingi na tangu mwaka 1995 vimekuwa vikishiriki uchaguzi Mkuu.

Hivyo katika uchaguzi Mkuu mwaka huu wa 2015 navyo vinajipanga kwa ajili ya kusimamisha wagombea katika nafasi ya madiwani,Wabunge na Rais lakini kwa mtazamo wangu kwa nafasi ya Diwani na Mbunge huko tutajua wakati ukifika watakaorudi sawa na wasiorudi sawa vile vile lakini kwa nafasi ya Rais tunaenda na Samia tu.

Sifanyi kampeni na sina uwezo huo lakini uliyoyafanya Rais yanathibitisha uwezo wako katika kulitumikia Taifa.Lakini hata tukisema tunamchagua Rais kutoka upinzani nani anasifa za kupambana na wewe Dk.Samia Suluhu Hassan au huyo Jamaa yao?

Wakati nahitimisha salamu zangu kwako Rais Samia uniruhusu niwakumbushe Watanzania kuhusu wewe kuwa ulizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja. Umeolewa na Bw. Hafidh Ameir na umejaaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.

Kuhusu elimu na mafunzo Dk.Samia Suluhu Hassan ulipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972. Baada ya hapo, ulijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha tatu, na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya Kidato cha Nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.

Mwaka 1983, ulipata Astashada katika Mafunzo ya Takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma.

Aidha, ulipita katika Taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya Utawala.

Baada ya hapo, ulijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya Juu ya Uchumi. Vilevile, ulipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Kuhusu uzoefu ndani ya Serikali ni kwamba Dk. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Ndugu Samia Suluhu Hassan wewe mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.







Nyadhifa nyingine ulizoshika ndani ya Serikali ni; Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano 2010/2015; Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2005/2010 na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2000/2005.




Mwaka 2014, ulihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge lililojadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania. Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu na Mwaka 1977 hadi 1983, Karani Masijala.

Kwa upande wa uzoefu ndani ya CCM ,Dk. Samia Suluhu Hassan uliingia katika siasa kama mwanachama wa CCM tarehe 10 Juni, 1987. Uliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama Mwakilishi wa Viti Maalum vya Wanawake hadi mwaka 2010.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, uligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwakilisha jimbo la Makunduchi, Zanzibar.

Mwaka 2002, ulichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, na vile vile, kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi; nyadhifa ambazo ameendelea kuzifanyia kazi hadi leo. Ndugu Samia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja; na alikuwa Mjumbe wa Kamati za Siasa Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja.

Kwa upande wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi, Ndugu Samia wewe ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia mwaka 1996 hadi leo. Aidha, umeshiriki katika kuandika Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara nne mfululizo kuanzia 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 na 2020/2025.

Baada ya maelezo hayo nitumie nafasi hii kukushukuru Rais Dk.Samia kwa kusoma salamu zangu kwako,najua unaweza usisome kila kitu au kuweka yote kichwani lakini bakia na hili tu Watanzania tunakupenda , tunakuombea maisha marefu.Tunafurahia uongozi wako.Heri ya mwaka mpya wa 2025 Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ,Mama wa Taifa la Tanzania, tabasamu lako ndio tabasamu letu Watanzania.

Ni mimi;0713833822

Post a Comment

0 Comments