Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameshuhudia utiaji saini mikataba 9 yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 4.7 ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na wakandarasi.
Hafla hiyo imefanyika leo, Januari 24, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Chama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Macha ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha na kutekeleza miradi ya maji mkoani Shinyanga, akielezea kuwa juhudi hizo zitasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi.
Macha ameeleza kuwa mikataba hiyo ni ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 4.7, ambapo vijiji 16 vitapata huduma ya maji, na vituo 18 vya kuchotea maji vitajengwa.
Amesema kuwa, kupitia utekelezaji wa miradi hii, Mkoa wa Shinyanga utaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 68 hadi asilimia 70 ifikapo mwisho wa mwaka 2025.
Macha amewataka wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa weledi na kumaliza kwa wakati, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wakandarasi kushirikiana na wananchi katika maeneo ya miradi, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwao.
Aidha, ameagiza RUWASA kuhakikisha inatoa taarifa ya utendaji kazi ya miradi kila baada ya tarehe 15 ya kila mwezi ili kutatua changamoto mapema na kuepuka mkwamo.
Pia, ametoa wito kwa wananchi kuzingatia utunzaji wa miundombinu ya miradi ya maji, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia maji ya safi na salama kutoka katika miradi hiyo.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela, amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo unatarajiwa kumalizika ndani ya miezi 6, na itakamilika ifikapo Juni 2025. Miradi hiyo itajengwa katika maeneo ya Kahama, Kishapu na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mhandisi Payovela amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Shinyanga, vijiji vingi sasa vimepata huduma ya maji, na kwamba serikali imeongeza fedha za ujenzi wa visima 20 vya maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kumaliza changamoto ya ukosefu wa maji.
Mhandisi Payovela ametaja changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika hasa katika Halmashauri ya Ushetu na Kishapu, pamoja na ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, jambo linalochelewesha utekelezaji wa miradi kwa wakati.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, ametoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha kuwa mabomba yanayotumika katika miradi ya maji ni bora ili kuepuka upotevu wa maji unaosababishwa na mabomba kupasuka mara kwa mara.
Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha na kutekeleza miradi ya maji, akieleza kuwa katika Jimbo la Msalala, asilimia 98 ya miradi ya maji imetekelezwa na wananchi wanafaidika na huduma hiyo.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mabala Mlolwa, na ametoa pongezi kwa watumishi na wakandarasi kwa kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, huku akisisitiza umuhimu wa uaminifu na weledi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mmoja wa wakandarasi, Mnandi Mnandi kutoka Kampuni ya URSINO LTD, ameishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapatia kazi, na ameahidi kwamba miradi hiyo itakamilika kwa wakati kama ilivyokubalika kwenye mkataba.
0 Comments