Vijana wa Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali Tarafa ya Iyula Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wametakiwa kuacha tabia ya kucheza mchezo wa pool table nyakati za asubuhi wakati muda huo wanapaswa kufanya shughuli rasmi za kujiingizia kipato kwa maendelo yao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Januari 14, 2025 na Polisi Kata ya Mlangali Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Robert Kasunga wakati akitoa elimu juu ya madhara ya kucheza mchezo huo masaa ya kazi kwa vijana wa Kijiji hicho baada ya kuwakuta wanacheza mchezo huo muda wa kazi ambapo walitakiwa kufanya kazi halali ili kujiingizia kipato kwa manufaa ya maisha yao.
"Acheni kushiriki michezo masaa ya kazi kwani mara nyingi inapelekea mfanye au mjiingize kwenye vitendo vya kihalifu, pia hupelekea kuwa tegemezi kwa wazazi na walezi wenu" alisema Mkaguzi Kasunga.
Kwa upande wao vijana hao wamelishukuru Jeshi la Polisi na wameahidi kushiriki kuimarisha ulinzi kwa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi na kushirikiana na jamii kuimarisha usalama katika kijiji hicho.
0 Comments