Na. Saidina Msangi, WF, Karatu, Arusha
Wananchi wa Wilaya ya Karatu jijini Arusha, wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia Taasisi za fedha zilizosajiliwa ambazo zinazingatia sheria, kanuni na taratibu katika huduma za fedha ili kujiepesha na watoa huduma za fedha wasio sajiliwa.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi H. Kolimba, alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliofika Wilaya ya Karatu jijini Arusha, kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Fedha, ili kuwawezesha wananchi kuwa na uelewa wa masuala ya fedha.
Mhe. Kolimba alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi ambayo haifuati sheria hivyo kusababisha malalamiko ya mara kwa mara na kusababisha wananchi kupoteza mali zao ambazo wameweka dhamana.
‘‘Tulishazungumza na watoa huduma za fedha na taasisi za fedha hapa wilayani na tukasisitiza kuwa mikopo wanayotoa isiwaumize wananchi na endapo tukigundua wanaenda kinyume na sheria tutawachukulia hatua za kisheria na tunasisitiza wananchi kutumia watoa huduma rasmi za fedha ili kuepuka mikopo isiyofuata sheria’’, alisisitiza Mhe. Kolimba.
Akizungumza kuhusu elimu inayoenda kutolewa na wataalamu wa Wizara ya Fedha wilayani humo alisema kuwa elimu hiyo itasaidia wananchi kupata uelewa wa haki na wajibu wa mtoa huduma katika utoaji wa mikopo ili kuwasaidia kuondokana na mikopo umiza.
Mhe. Kolimba alisema kuwa ana imani elimu itakayotolewa kwa wananchi itawaongezea uelewa zaidi wa kutambua haki zao ikiwemo kufahamu taratibu za mikopo ikiwemo kiasi cha riba watakachotozwa na taasisi ya fedha katika mikopo wanayochukua kabla ya kuchukua mkopo.
‘Natoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo haya ya kutoa elimu kwa wananchi na pia nimpongeze Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo haya kuhakikisha kuwa elimu hii ya fedha inawafikia wananchi ili kuondokana na changamoto za kiuchumi‘’, aliongeza Mhe. Kolimba.
Aidha, alisisitiza wananchi wilayani Karatu kuhakikisha kuwa wanapochukua mikopo kwa wenye wenza wawashirikishe ili inapotokea changamoto katika urejeshaji wa mkopo husika waweze kushirikiana kurejesha lakini pia kuepuka migogoro ya familia endapo mwenza asiposhirikishwa na mkopaji akishindwa kurejesha mkopo kwa wakati.
Akizungumza kuhusu programu ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu jijini Arusha, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya alisema kuwa Wizara inatekeleza programu hiyo ili kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha Wananchi kutumia huduma za fedha zilizo rasmi.
Alisema kuwa katika wilaya ya Karatu timu hiyo itawafikia wajasiriamali, wafanyakazi, watoa huduma za fedha, wahamasishaji wa huduma ndogo za fedha, wadau wa utalii pamoja na wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
‘‘Katika awamu ya tatu ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi iliyoanza mwezi Januari 2025, mikoa tunayotarajia kuifikia ni mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Mara’’, alieleza Bw. Kibakaya.
Alifafanua kuwa Program ya kutoa elimu kwa Umma ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo Sekta ya Fedha 2020/21 - 2029/30 ambapo unalenga kufikia wananchi asimia 80 hadi kufikia mwaka 2025/26 pamoja na utekelezaji wa Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma ya mwaka 2020/21 - 2025/26.
Bw. Kibakaya alibainisha kuwa maeneo yatakayotembelewa katika wilaya ya Karatu ni Kata ya Endabash, Mang’ola, Baray, Rhotia kati na Mbulumnbulu ambapo mada zitakazowasilishwa ni usimamizi wa fedha binafsi, akiba, mikopo, bima, uwekezaji wa fedha pamoja na kupanga kwa ajili ya maisha ya uzeeni.
Awamu ya kwanza ya utoaji wa elimu ya fedha iliyoanza mwezi mei mwaka 2024 ilifikia mikoa 12 na halmashauri 62 ambapo makundi mbalimbali yalifikiwa ikiwamo wajasiriamali, watumishi wa umma na binafsi, wakulima, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, wahamasishaji wa huduma ndogo za fedha pamoja na watoa huduma za fedha.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dadi H. Kolimba, akipitia moja ya vipeperushi alivyokabidhiwa na Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, wakati timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ilipowasili Wilaya ya Karatu kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba, akizungumza na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha wakati ilipowasili wilayani Karatu kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, ofisini kwa mkuu wa Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi H. Kolimba (wa tatu kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, wakati walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini. Kulia ni Afisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya akifuatiwa na Joshua Alinanuswe Mwamsojo, Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Karatu. Kushoto ni Afisa Sheria Mwandamizi Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, Katibu Tawala wilaya ya Karatu Dkt. Lameck Karanga na Bw. Renatus Lucas, Mchumi Mchumi wa Wizara ya Fedha.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa wilaya ya Karatu, wakati timu hiyo ilipowasili wilayani Karatu kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, katika ukumbi wa KDA, Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Afisa Sheria Mwandamizi Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa wilaya ya Karatu, wakati timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, katika ukumbi wa KDA, Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karatu, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliowasili wilayani Karatu kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, katika ukumbi wa KDA, Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Afisa Sheria Mwandamizi Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa maelekezo kwa Bw. Aboubakar Iddi, kuhusu namna sahihi ya kupata mikopo, haki za mteja na wajibu wa mtoa huduma, wakati timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, katika ukumbi wa KDA, Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya (kulia), Afisa Mahusiano Benki ya NMB Karatu Bw. Kiringo Kessy na Bw. Jackson Mwambola kutoka benki ya NBC (kushoto), wakimkabidhi zawadi ya fulana aBi. Eliupendo Martin, baada ya kujibu maswali kuhusu akiba ya uzeeni, wakati timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini, katika ukumbi wa KDA, Wilaya ya Karatu, Jijini Arusha.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Karatu, Arusha)
0 Comments