Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Sumbawanga Mkoa wa Rukwa Mhe. Deus Sangu ametoa rai kwa wasimamizi wa magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) kuifanya kazi hiyo ya uratibu wa magari hayo kwa weledi na ufanisi ili kuokoa maisha na kulinda afya za wananchi wa jimbo hilo.
Mhe. Sangu amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi gari ya kubebea wagonjwa kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kituo cha Afya Kipeta Kata ya Kipeta -Jimbo la Kwela katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
“Tunamshukuru Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa moyo wa dhati na wa upendo kwetu hususani wananchi wa Kata ya Kipeta na Kilangawana ametoa gari ya kubebea wagonjwa, hii ni heshima kubwa kwetu na hatuna budi kumuombea kwa Mungu ili aendelee kutuongoza na kutujali zaidi” alisema Mhe. Sangu.
Aidha, alibainisha kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa vifaa tiba na kujenga vituo vya afya na zahanati kila Kijiji hususani katika Jimbo la Kelwa kwa lengo kuendelea kuboresha afya za wananchi wake.
Alisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika Jimbo la Kwela mathalani ujenzi wa vituo vya Afya, Zahanati, Barabara, Maji na Shule ni jithada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaelenga kuimarisha afya na ustawi wa wananchi wa Jimbo la Kwela.
Aidha, Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wa jimbo lake kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokea maombi ya magari ya wagonjwa na kwa upendo mkubwa amejibu maombi hayo ndani ya muda mfupi ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2024 ametoa magari manne (4) yenye thamani ya jumla ya milioni 800 na bado ameahidi kuendelea kuleta maendeleo zaidi katika jimbo hilo.
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga Dkt. Yahya Msuya amemshukuru Mhe. Sangu kwa kufikisha kilio chao cha mahitaji ya gari ya kubebea wagonjwa na ndani ya muda mfupi yamepatikana.
Dkt. Msuya ameongeza kuwa maelekezo ya Mhe. Sangu yamepokelewa na ameahidi gari hiyo kuhudumia wananchi wa Kata ya Kipeta na Kilangawana na atahakikisha wananchi wanapata huduma bora za kiafya. Vilevile, Dkt. Msuya ameahidi kuwa atasimamia vyema magari hayo ili yafanye kazi kama ilivyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wote katika jimbo la Kwela, Halmashauri ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa jumla.
Hafla hiyo imehuduriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Viongozi wa chama na Serikali.
0 Comments