Ni kijana kutoka Jijini Mwanza, Wilaya ya Magu mwenye Elimu ya darasa la Saba pekee, hana Elimu ya kutisha lakini usishangae ukisikia Lugumi ni Daktari (PhD) udaktari wa heshima kwakuwa anastahili hilo kwa kiwango kikubwa kutokana na namna anavyojitoa kwa jamii.
Tofauti na Wafanyabiashara wengine, ukisikia habari zao mitandaoni ni mambo tofauti lakini kwa Lugumi imekuwa tofauti sana ambapo mwishoni mwa mwaka 2024 mwezi Disemba aliibua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kuonesha sehemu ya nyumba anazojenga kwaajili ya watoto Yatima anao walea katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Bilionea Saidi Lugumi anaeleza kwa sasa kuna watoto yatima zaidi ya 800 kutoka maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam ambao anawahudumia kwa kila kitu ikiwemo chakula, mavazi, malazi, elimu, afya l, na hiyo inatokana na wito alionao kutoka kwa Mwenyezi Mungu na si vinginevyo.
Desemba 25, 2024 katika kusherekea sikukuu ya Krismasi alijumuika na watoto wake mtaa wa Msufini, wilaya ya Kinondoni kwa ajili ya kushirikinao dua na kisomo maalum sambamba na kushirikinao chakula cha pamoja alichokiandaa kwa ajili yao
Sambamba na hilo, katika kuboresha makazi yao Lugumi alisema kwa sasa anajenga majengo sita (6) ya ghorofa huku malengo yakiwa ni kujenga ghorofa nane (8) kwa ajili ya watoto hao, kwenye maeneo tofauti ya jiji hilo, ambapo jengo moja kati ya hayo linajengwa eneo hilo la Msufini.
"Hii ni nyumba yao (jengo la ghorofa), nyumba kama hizi ziko sita (6) lakini tumeanzia hapa kwa sababu nyumba hii iko mbioni kumalizika, chakula tutakula na wao hapa, na wenyewe wameweza kuwa na furaha kuona sehemu yao, kila kituo kinatarajiwa hakitazidi kukaa watoto 100, unaona nyumba kama hii ni watoto 100 tu na kwa namna Mungu anavyonijaalia nitazidi kuongeza, kwa sasa tumepanga nyumba kama tatu na nyingine tumenunua lakini bado hazitoshi", alisema Lugumi.
Lugumi anaeleza kuwa alianza kulea watoto hao na alipata maono hayo mnamo mwaka 2013 ambapo ni takribani miaka 12 sasa na amesisitiza kuwa yuko tayari apoteze kitu chochote lakini sio kuwapoteza watoto hao.
Kila Kituo kuna madaktari na maafisa Ustawi wa Jamii ambao wapo kwaajili ya kuwahudumia watoto hao ukiachana na suala la mavazi na malazi watoto hao wanasomeshwa mpaka ngazi za juu za Elimu na kuendelea na maisha yao na wengine hupatiwa mitaji ya Biashara huku wengine wakianza ajira zao.
Lugumi anasimulia kuwa sio kwamba siku zote wanapitia raha na wanae, kuna vipindi hali inakuwa sio nzuri na wanalazika kula wanachokipata.
Viongozi wa Dini wamepongeza juhudi za Lugumi, akiwemo Mtume Boniface Mwamposa 'Buldoza' wa Kanisa la Inuka Uangaze amempongeza mfanyabiashara Lugumi kwa kujenga maghorofa matano kwa ajili ya watoto yatima.
“Ninampongeza Lugumi, ni jambo jema lenye roho ya kumcha Mungu,” alisema Mwamposa.
Majengo hayo, yanayotarajiwa kukamilika Machi mwaka huu, yatanufaisha zaidi ya watoto 800 wenye mahitaji maalum jijini Dar es Salaam.
Saidi Lugumi ni mfanyabiashara mkubwa nchini Tanzania, anayejulikana zaidi kama Mkurugenzi Mtendaji wa Lugumi Enterprises Limited.
Lakini pia kupitia kampuni ya Tactical Defencs (T) Limited ni wakala wa makampuni makubwa ya silaha duniani.
Lakini pia, kampuni yake inajihusisha na huduma za uchapishaji wa vifaa vya ki-ofisi, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) na hajawahi kuwa na Biashara nyingine tofauti na ilivyodaiwa kuwa anajihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya.
Maisha yake binafsi Lugumi amekuwa sio Mtu wa kuweka wazi sana familia yake, lakini amewahi kukiri kuwa na watoto Saba (7) ambao ni wa kwake wa kuwazaa na wapo sehemu tofauti tofauti, huku akikanusha taarifa za kuwahi kumuoa binti aliyedaiwa kuwa ni familia ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Saidi Mwema.
0 Comments