Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KIASI cha shilingi Bilioni 5.3 zapatikana katika zoezi la uuzaji wa hatifungani ya miundombinu (Samia Infrastructure Bond), Mkoa wa Tanga iliyozinduliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za mjini na vijijini (TARURA) Mkoa wa Tanga.
Fedha hizo zimebainishwa katika uzinduzi wa mauzo ya hatifungani hiyo, zoezi linalotekelezwa kwa mashirikiano ya Taasisi hizo ikiwa ni maalumu katika mapinduzi ya kimiundombinu ya nchi ambapo wananchi wote wanapaswa kushiriki.
Akiwasilisha kwa niaba ya Meneja wa Biashara Kanda ya Kaskazini, David Peter, Meneja wa CRDB Mkoa wa Tanga John Mtani, amesema lengo la hatifungani hiyo ni kutatua tatizo la kifedha linalokabili Taasisi katika utekelezaji wa barabara.
"Hatifungani hii tumeanza kuiuza Novemba 29, na tutarndelea hadi Januari 17 mwaka huu, tukitoa siku za mapumziko tunabakiwa na siku 5 kuhakikisha tunafunga zoezi hili, lakini kwenye solo la mitaji itaorodheshwa Februari 10 na itakuwa kwa miaka mitano hadi Februari 10, mwaka 2030" amesema.
Aidha amebainisha faida kadhaa atakazopata mwekezaji baada ya kununua hatifungani, ikiwemo ya kupata malipo ya gawio kwa asilimia 12 ambayo yatafanyika mara nne kwa mwaka.
Amesema kiwango cha chini cha uwekezaji ni shilingi Laki tano na hakuna kiwango cha juu, lakini pia uwekezaji huo unategemewa kuongeza kasi kwa TARURA katika utekelezaji wa ujenzi wa barabara.
Mtani ametoa wito kwa wananchi wote mkoani humo kujitokeza kabla ya tarehe ya mwisho, kuunga mkono juhudu za serikali kwa kununua hatifungani ili kuharakisha maendeleo katika utekelezaji wa miundombinu ya barabara.
0 Comments