Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo,akizungumza kwenye Kipindi cha mahojiani cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC kilichofanyika leo Januari 22,2025 katika ofisi za Kituo hicho jijini Dar es Salaam.
Na.Mwandishi Wetu
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema Serikali ya Tanzania inaandika historia katika uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini kwa kuzindua zoezi la ulipaji wa fidia kiasi cha shilingi bilioni 14.48 kwa wananchi watakaopisha Mradi wa Magadi Soda uliopo Engaruka, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.
Ameyasema hayo aliposhiriki Kipindi cha mahojiani cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC kilichofanyika Januari 22,2025 katika ofisi za Kituo hicho Dar es Salaam.
Dkt.Jafo amesema kati ya kiasi hicho jumla ya shilingi bilioni 6.2 zitatolewa moja kwa moja kwa Wananchi 595 kutoka vijiji vinne vya Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni na fedha iliyobaki itagharamia ujenzi wa Miundombinu itakayoharibika kupisha mradi huo.
Aidha Dkt.Jafo amesema mradi huo una manufaa makubwa kwa Taifa kwani magadi soda ni malighafi muhimu kwenye Viwanda vingi kuongeza ajira, kukuza uchumi wa viwanda na kuendeleza au kujenga viwanda ikiwemo viwanda vya madawa, kemikali, viwanda vya kuzalisha vioo, sabuni, rangi, karatasi, kusafishia mafuta ya petroli, kusafishia madini,kutengenezea mbolea, na kusafishia maji.
Dkt.Jafo pia ametoa rai kwa Watanzania kupuuza taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa kupitia mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo zinazodai kuwa una athari kubwa ya kimazingira ambapo amesema mradi ambao hapo awali ulisemwa una athari ulikuwa katika Ziwa Natroni lakini mradi wa sasa wa unafanyika katika Bonde la Engaruka na kazi hii imefanyika kwa umakini na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC )limepata cheti maalumu cha tatmini ya Mazingira hivyo Taifa halitarudi nyuma kwenye uwekezaji ili kuhakikisha Vijana wanapata ajira.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo,akizungumza kwenye Kipindi cha mahojiani cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC kilichofanyika leo Januari 22,2025 katika ofisi za Kituo hicho jijini Dar es Salaam.
0 Comments