Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Dkt. Mark Bristow (katikati waliokaa), Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (wa tatu waliokaa), Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Petro Kurate (wa pili waliokaa), viongozi wa kata na vijiji, na wafanyakazi wa mgodi wa North Mara wakifurahia picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya mifano ya hundi za malipo ya 'service levy' na mrabaha.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Dkt. Mark Bristow akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi bilioni 3.7 kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika ukumbi wa mikutano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
Wawakilishi wa vijiji wakipokea fedha za malipo ya mrahaba wakati wa mkutano huo
Wawakilishi wa vijiji wakipokea fedha za malipo ya mrahaba wakati wa mkutano huo
Viongozi wa halmashauri, kata na vijiji wakiwa katika kikao na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Dkt. Mark Bristow (hayupo pichani) ambapo Mgodi wa Dhahabu wa North Mara malipo ya 'service levy' kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mrabaha kwa vijiji vitano.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Barrick katika mkutano huo
***
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) shilingi bilioni 3.709, ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma (service levy) ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Wakati huo huo, mgodi huo umelipa kwa vijiji vitano wilayani humo gawio la mrabaha la shilingi bilioni 1.718 ambazo ni malipo ya robo ya nne ya mwaka 2024.
Vijiji hivyo na kiasi cha fedha kilichopokewa kikiwa kwenye mabano ni Genkuru (749,488,891), Nyangoto (635,141,742), Kerende (195,749,927), Nyamwaga (95,529,025) na Kewanja (42,254,479).
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Dkt. Mark Bristow, amekabidhi mifano ya hundi za malipo hayo ya ushuru wa huduma na mrabaha kwa viongozi husika , wakati wa kikao chake na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) inayoundwa kwa sehemu kubwa na viongozi wa vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo.
Viongozi wa halmashauri na vijiji wameushukuru mgodi wa North Mara na kuahidi kusimamia vizuri matumizi ya mabilioni hayo ya fedha ili kuchochea maendeleo ya wananchi, hasa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za kijamii.
“Tunaushukuru sana mgodi kutupatia fedha hizi, na sisi kama viongozi tunaahidi kwamba zitakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Petro Kurate.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Meneja Mkuu wa Mgodi, Apolinary Lyambiko na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye amewataka viongozi wa halmashauri na vijiji kushirikisha wananchi katika matumizi ya fedha hizo.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
0 Comments