Ticker

6/recent/ticker-posts

VINARA 16 WAPATIWA TUZO KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Na Mwandishi wetu 

Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na UNFPA limetoa tuzo kwa vinara 16 wa kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia ambao wametumia ujuzi na taaluma zao  katika kupinga ukatili huo kwa mwaka 2024.

Hayo yalisemwa jana  na Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF,Anna Kulaya wakati wa ugawaji wa tuzo hizo jijini Dar es Salaam amesema lengo la kutoa tuzo hizo ni  kutambua ustahimilivu, ujasiri, na azma ya wale ambao wamechagua kusimama mstari wa mbele katika vita vya kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini.

Amesema ukatili wa kijinsia sio suala la maumivu au mateso kwa mtu binafsi,bali ni tatizo la kijamii ambapo kwa Tanzania ni janga la kitaifa linalovunja muundo wa jamii zetu.

Amesema  kupitia vinara hao 16 wanawakukumbusha kwamba mabadiliko huanzia kwa wale wanaothubutu kuchukua hatua, hivyo kupitia kazi zao  zimeakisi aina ya ujasiri na huruma inayobadilisha maisha na jamii.

''Inatufundisha sote kwamba hata mbele ya changamoto kubwa,daima kuna fursa ya kuchukua hatua,kuponya na kuwawezesha wengine,''alisema na Kuongezea

''WiLDAF inapotoa tuzo hizo ni ishara ya kukumbuka kwamba kazi hiyo ya kupambana na ukatili wa kijinsia bado haijaisha kwani ukatili wa kijinsia unabaki kuwa changamoto inayodumu,''alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya WiLDAF,Dkt.Monica Mhoja,amesema wanafurahi katika kukamilisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kutoa tuzo kwa baadhi ya watu binafsi wanawake  na wanaume ambao wamekuwa chachu kuleta maendeleo ndani na nje ya nchi.

Amesema vinara hao 16 wamejitahidi wao wenyewe kwa hamasa mbalimbali kuweza kuhakikisha wanapambana na kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo mbalimbali ikiwemo sehemu zao za kazi,majumbani na hata mitandaoni.

''Tunavinara mbalimbali ambao wamepata Tuzo leo ikiwemo wale waliopo serikalini kama Mapolisi ambao wamekuwa chachu katika madawati ya jinsia kuhakikisha haki za wanawake,vijana katika masuala ya ukatili wa kijinsia zinatendewa haki,''amesema.

Akiongea kwa niaba ya vinara wengine waliopata Tuzo hizo, Mzee wa Kimila kutoka Mkoani Arusha Wilayani Ngorongoro, Alaigwanani Parmira ameishukuru WiLDAF kwa utoaji wa tuzo hizo na kutambua nafasi zao katika jamii.''Umasaini haijawahi kutokea watu kupatiwa Tuzo kama hiyo kwa ishara ya kuwakumbuka,''alisema.

Amesema kwa sasa hali ya ukatili wa kijinsia imepungua tofauti na miaka ya nyuma ambapo watoto walikuwa hawaendi shule,Tohara za wasichana kwa sasa imepungua na wanawake kunyanyasika hakuna tena.

Nuru Awadhwi Kinara kwa watu wenye ulemavu, amesema tuzo hiyo ameipokea baada ya kuona alikuwa na mzigo mkubwa wa kupambana katika kutoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia.

Amesema Wildaf imefanya kitu cha kuvutia na kufanya wanawake wengine wenye ulemavu wengi kuingia katika kufanya kazi na kupambana kutokomeza ukatili wa kijinsia.

''Pamoja na sisi tunapambana kutoa elimu lakini bado kila mmoja anawajibu kama ni mzazi,mtumishi au mtoa huduma katika jamii anapaswa kuhakikisha anatokomeza ukatili wa kijinsia na kuleta usawa wa kijinsia Tanzania katika kila eneo ambalo mtu yupo,"amesisitiza 

Miongoni mwa tuzo hizo zilizotolewa ni pamoja na Tuzo ya  Kupinga Ukatili Mitandaoni,Kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu,Kutetea haki za wajane,Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Waandishi wa Habari,Tuzo ya Kiongozi wa Kimila katika  kupinga ukatili wa kijinsia Ngorongoro na Kiongozi wa dini Kinara wa kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Tuzo nyingine zilizotolewa ni Tuzo ya  Kinara wa Kupinga Ukeketaji wa Wanawake,Kinara wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia  pamoja na Kinara wa kuzuia na kupinga ukatili wa kingono kupitia sanaa na ubunifu.

   


Post a Comment

0 Comments