WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki kuendelea kujadili changamoto katika utoaji haki na kuweka mipango endelevu ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo kupitia mikutano yake.
Ametoa wito huo leo (Disemba 03, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Ishirini na Moja wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hotel ya GranMelia jijini Arusha.
“Mkutano huu pamoja na mambo mengine ni muhimu kujadili masuala muhimu ya Kitaifa na Kikanda katika mfumo wa utoaji haki, pia nina imani kupitia mkutano huu mtajadili umuhimu wa kuimarisha na kuboresha mifumo ya utoaji haki na kutumia ukuaji wa teknolojia ili kuboresha kwenye ufanisi wa majukumu yenu”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Majaji na Mahakimu hao kujadili namna mifumo ya utoaji haki inavyoweza kuwa chachu ya ushirikiano wa kikanda na ukuaji wa uchumi. “Mnapaswa kujadili namna mifumo ya utoaji haki inavyoweza kusaidia katika kukuza mtangamano wa kikanda na ukuaji wa uchumi”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya maboresho na mapitio ya mifumo ya utoaji haki yenye lengo la kuimarisha ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
“Serikali yetu, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, tumefanya maamuzi muhimu ya kisera kijamii na kiuchumi ambayo yanaakisi mwelekeo wetu wa maendeleo wenye lengo la kuboresha ustawi na ustawi wa watu wa Tanzania”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Kupitia Mpango ya Maendeleo ya Miaka Mitano, Serikali ya Tanzania imedhihirisha dhamira yake ya kuboresha mfumo wa utoaji haki. Mnamo 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliteua "Tume ya Rais ya Haki Jinai" yenye lengo la kuleta mageuzi katika mfumo wa haki za jinai.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa Serikali inatahamini kazi kubwa zinazofanywa na Mahakimu na Majaji kwa kuwa wao ni kitovu cha amani na utulivu.
Kw Upande wake Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amesema kuwa kupitia mkutano huo watapata nafasi ya kujifunza na kubalishana uzoefu. “Tumeweza kubadilishana uzoefu katika mifumo ya haki jinai na namna tunavyoweza kuitumia teknolojia katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa ufanisi na haraka bila ucheleweshaji”.
0 Comments