Ticker

6/recent/ticker-posts

WATANZANIA WAHIMIZWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUSOMA VITABU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Sayansi na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu ili kuibua fursa za kimaendeleo na kuacha tabia ya kutumia vitabu kama sehemu salama ya kuhifadhia fedha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vilivyoandikwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Mushi amesema, vitabu hivyo ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo na elimu nchini ambapo ameipongeza SUA na waandishi wa vitabu hivyo kwa jitihada zao za kuleta tija kwa jamii kwa kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali.

“Wizara inatamani kuona wanataaluma nchini wanachukua jukumu la kuandika vitabu vinavyojikita katika tafiti na kuendana na mtaala mpya wa elimu unaolenga kukuza stadi za amali. Kwa kuandika vitabu, wanataaluma wanaweza kuhifadhi mawazo yao ya kibunifu na kusaidia jamii kutatua changamoto,” amesema Prof. Mushi.

Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia, SUA, Prof. Samwel Kabote, amesisitiza kuwa vitabu hivyo vina uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na elimu nchini, na kama mawazo yaliyoandikwa yakitekelezwa kwa vitendo, yatachangia kupunguza umasikini.

Josephine Ng’ang’a, Mkurugenzi wa RECODA (Research, Community and Organizational Development Associates), ameeleza kuwa mojawapo ya vitabu hivyo kinachotumia mfumo wa RIPAT, kinalenga kuwapa wakulima maarifa ya kutumia teknolojia zilizofanyiwa tafiti ili kuleta maendeleo. Alisema kuwa vitabu hivyo pia vinaweza kutumika na watafiti na wadau wa maendeleo vijijini katika kutekeleza miradi yenye tija kwa jamii.

Dkt. Onesmo Nyinondi, mmoja wa waandishi wa vitabu hivyo na Mhadhiri Mwandamizi wa SUA, alisema changamoto kubwa ya wanafunzi kuandika makala na majarida kwa umahiri ndiyo ilimhamasisha kuandika kitabu chake.

Aliongeza kuwa vitabu ni njia bora ya kutoa maarifa kwa wanafunzi na watafiti.

Uzinduzi wa vitabu hivyo, umeofanyika katika kampasi ya Edward Moringe SUA, mkoani Morogoro, umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na elimu, wakiwemo viongozi wa SUA, watendaji wa serikali, na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali kama RECODA.

Vitabu hivyo vinatarajiwa kuchangia maendeleo endelevu kwa kusaidia wakulima, watafiti, na wadau wa elimu nchini.

Post a Comment

0 Comments