Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Desemba 13, 2024, imekuwa ni siku ya kihistoria kwa waandishi wa habari na wadau wa habari Mkoa wa Mwanza, walipokutana katika hafla ya kipekee ya Media Stakeholders Night Gala 2024.
Hafla hii, iliyofanyika katika ukumbi wa Mwanza Hotel, ilikusudia kuwaunganisha waandishi wa habari na wadau wao ili kusherehekea mafanikio ya mwaka mzima, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya habari.
Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe. Christopher Ngubiagai, ambaye alikuwapo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ngubiagai amesisitiza kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwa na uwajibikaji katika kazi zao, akiwashauri kutumia kalamu zao kwa usahihi na kuzingatia maadili ya uandishi ili kuepuka migogoro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (Mwanza Press Club - MPC), Bw. Edwin Soko, ameelezea furaha yake kwa kuona wadau wa habari kutoka sekta mbalimbali wakikusanyika pamoja.
Amesema kuwa hafla hii ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka wa MPC, ambao unalenga kuimarisha ushirikiano na kudumisha uhusiano mzuri kati ya waandishi wa habari na wadau wao.
Hafla hii imehudhuriwa na wadau wa habari kutoka taasisi mbalimbali muhimu, ikiwa ni pamoja na Tashico, NHIF, TCRA, NSSF, TIRA, Jeshi la Polisi, Bodi ya Pamba na TCB.
Ushiriki wa taasisi hizi umeonyesha utayari wa sekta zote kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa taarifa sahihi na za kuaminika zinawafikia wananchi.
Hafla ya Media Stakeholders Night Gala 2024 limekuwa ni tukio la kipekee ambalo limeongeza msisitizo wa umoja na ushirikiano kati ya waandishi wa habari na wadau wa tasnia ya habari, huku wakijadiliana kuhusu namna bora ya kuendeleza tasnia ya habari na kupiga hatua katika kuleta maendeleo kwa jamii.
0 Comments