Ticker

6/recent/ticker-posts

MIRADI YA PEPFAR/CDC NA USAID YACHANGIA JITIHADA ZA SERIKALI KUTOKOMEZA UKIMWI

*Ni kwenye miradi ya Ukimwi,Kifua Kikuu,Uchunguzi wa Saratani ya Kizazi
Na Chalila Kibuda 

Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), limeshirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani.

Maadhimisho ya kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Maji Maji, mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI."

Katika maadhimisho haya, THPS imeendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa upimaji wa VVU, kuepuka tabia hatarishi, kuzingatia tiba ya VVU, na kuhamasisha uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

Katika kipindi cha Oktoba 2023 hadi Septemba 2024, THPS kupitia Mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua ilitoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa watu 1,170,902, ambapo 17,989 walibainika kuwa na VVU.

Hayo yalibainishwa na Dkt. Eva Matiko, Mkurugenzi wa Miradi wa THPS, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, watu 190,311 walipata huduma ya dawa za kufubaza makali ya VVU kupitia vituo vya afya 350 vilivyofadhiliwa na mradi huu.

Vilevile, watu 1,731 walikamilisha matibabu ya kinga dhidi ya Kifua Kikuu, na wanawake 67,914 wanaoishi na VVU walipokea huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga.

THPS pia imejizatiti kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

“Mradi huu ulitoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa wahanga 52,978, ambapo 47,633 walikuwa wahanga wa ukatili wa kimwili au kihisia, na 5,345 walikuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia”, alisema Dkt. Matiko.

Pia, THPS ilitoa huduma za tohara kinga kwa wanaume 165,711 katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga.

Aidha, wasichana rika balehe na wanawake vijana 33,313 walinufaika na mpango wa DREAMS (Determined, Resilient, Empowered, Free from AIDS, Mentored and Safe) katika mkoa wa Shinyanga, ambao unalenga kutoa huduma za afya na kuzuia maambukizi ya VVU kwa wasichana na wanawake vijana.

Kwa upande mwingine, kupitia mradi wa USAID Police and Prisons Healthcare, kuanzia Oktoba 2023 hadi Septemba 2024, THPS ilitoa huduma za upimaji wa VVU kwa watu 89,602, ambapo 2,030 waligundulika kuwa na VVU.

Kadhalika, watu 1,362 waligundulika kuwa na Kifua Kikuu na walipatiwa matibabu stahiki.

Watu 2,697 walianzishiwa na kukamilisha dawa kinga dhidi ya Kifua Kikuu, wakiwemo watu wanaoishi na VVU na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao walikuwa wanaishi na watu wenye ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Huduma zinazotolewa na THPS kwa ufadhili wa PEPFAR kupitia CDC na USAID zina mchango mkubwa katika jitihada za serikali za kupambana na UKIMWI na kufikia malengo ya kimataifa kudhibiti UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Tanzania Healthy  Promotion Services (THPS) Dkt.Eva Matiko akizungumza na waandishi wa Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani katika viwanja vya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukimwi wa Jeshi la Magereza Makao Makuu Mrakibu Mwandamizi wa Jeshe hilo Adili Kachima akizungumza katika akizungumza kuhusiana mafanikio ya Mradi wa Polisi na Magereza unaofadhiliwa na USAID kuratibiwa na THPS katika kuwafikia katika huduma upimaji wa VVU na Kifua Kikuu kwa Familia za Magereza na Wafungwa pamoja na Mahabusu
Meneja Ufundi wa Afya wa Polisi na Magereza wa THPS Dkt.Geofrey Tarimo akizungumza kuhusiana na mradi ulivyoleta matokeo kwa magereza  na Polisi katika upimaji wa VVU pamoja na Kifua Kikuu
Waziri wa Afya Jenista Mhagama akizungumza na Mkurugenzi wa Miradi wa THPS Dkt.Eva Matiko wakati alipotembelea Banda hilo katika maadhimisho  ya Siku ya Ukimwi Duniani Songea mkoani Ruvuma.
Wanafunzi  wakipata maelezo  katika bandaa THPS wakati walipotembelea katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi  Duniani.

Post a Comment

0 Comments