Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amemwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom, akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam, ambapo Tanzania imepongeza na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Jumuiya hiyo kuanzisha Mfuko wa Kikanda wa Maendeleo wa SADC.
Katika Hotuba yake fupi, Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa, ili SADC iweze kusonga mbele na kuwa na uchumi endelevu na stahimilivu, ni muhimu kutekeleza miradi ya Kimkakati ya Kikanda, kwa kutafuta rasilimali fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kwa gharama nafuu ikiwemo kuutumia Mfuko wa Kikanda wa Maendeleo wa SADC utakapoanzishwa.
Aidha, Dkt. Natu Mwamba, akisoma hotuba hiyo ya Mhe. Waziri wa Fedha, alibainisha kuwa ni ukweli usiopingika kwamba nchi nyingi wanachama wa SADC zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni kutoka kwa Mashirika makubwa ya kifedha duniani, kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama za ukopaji katika masoko ya fedha ya kimataifa, kupungua kwa misaada na mikopo nafuu, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Alitoa wito kwa nchi wanachama kuchangia mtaji wa Mfuko wa Maendeleo wa SADC ili kuanza utekelezaji wake na kwamba Tanzania inaunga mkono pendekezo la nchi wanachama kupewa uhuru wa kuchagua njia yoyote inayoona inafaa na bora ili kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuchangia mtaji huo.
0 Comments