Ticker

6/recent/ticker-posts

Wizara ya Nishati, Equinor wakutana Afrika Kusini

Wizara ya Nishati Tanzania imekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya Equinor Tanzania AS kujadili, pamoja na mambo mengine, maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (LNG).

Mazungumzo hayo yalifanyika Novemba 05, 2024 Jijini Cape Town – Afrika Kusini wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika, mkutano ulioleta pamoja wadau zaidi ya 5000 kutoka ndani na nje ya Afrika.

Kwa upande wa Wizara ya Nishati, kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi asilia, Dkt. James Mataragio na Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mha. Joyce Kisamo.

Miongoni mwa viongozi kutoka Taasisi za Wizara walioshiriki ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bw. Mussa Makame.

Ujumbe wa Equinor uliongozwa na Makamu wa Rais wa Equinor Kanda ya Bara la Afrika, Bi. Nina Birgitte Koch.

Akifungua kikao hicho, Dkt. James Mataragio alisema kuwa Wizara ipo tayari kusikiliza na kuchukua mapendekezo yatakayotolewa na kampuni hiyo yanayolenga kuwezesha utekelezaji wa mradi kwa wakati.

“Awali ya yote niishukuru Equinor Tanzania kwa kuomba kikao hiki muhimu na Wizara. Tunatambua kuwa utekelezaji wa mradi wa LNG unahusisha wadau wengine ambao hawapo hapa ila hiyo haizuii wizara kukutana na kumsikiliza mdau mmoja mmoja” alisema Mataragio.

Kwa upande wa Equinor, pamoja na kueleza masuala ya LNG na kutoa ushauri kwa Wizara, Bi. Nina alitumia fursa hiyo pia kutoa taarifa ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa kampuni hiyo nchini Tanzania ambapo alisema nafasi ya Maneja wa Equinor Tanzania ambayo kwa sasa inashikiliwa na Dr. Unni Fjaer itachukuliwa na Bi. Hilde Nafstad kutoka Norway.

Kampuni ya Equinor Tanzania AS ni miongoni mwa wabia wanaohusika katika utekelezaji wa mradi wa LNG nchini Tanzania.

Mradi huo unaolenga kuendeleza gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi Kusini mwa Tanzania, unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani takribani Bilioni 42.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio (wapili kushoto) akiongoza kikao kati ya  Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio (katikati) akiongoza kikao kati ya  Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio (mwenye miwani katikati) akiongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Katikati upande wa Equinor ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bi. Nina Birgitte Koch. 
Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio (watatu kushoto) akiongoza kikao kati ya  Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.

Post a Comment

0 Comments