Ticker

6/recent/ticker-posts

WATAALAM, MAMA NA WATOTO WAADHIMISHA SIKU YA MTOTO NJITI MUHIMBILI MLOGANZILA.

Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila imeadhimisha siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati duniani kwa kuwakutanisha wataalam, mama na watoto wao kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo na malezi ya watoto hao.

Akiongea katika kilele cha siku hiyo MNH Mloganzila Daktari Bingwa wa Watoto ambaye amebobea kwa watoto wachanga, Dkt. Lucy Mpayo amesema mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati akihudumiwa vizuri anakua bila shida yoyote kwakuwa kuzaliwa kabla ya wakati sio ugonjwa.

Dkt. Lucy amewashauri wanawake wenye ujauzito kuhudhuria kliniki mapema na kuongeza kuwa inashauriwa kuhudhuria kliniki angalau mwezi mmoja baada ya ujauzito ili kupata ushauri wa wataalam ambao utamsaidia mtoto na mama kwani baadhi ya sababu zinazosababisha mama kupata mtoto kabla ya wakati zinaepukika.

“Baadhi ya sababu zinazosababisha mama kuzaa mtoto kabla ya wakati ni pamoja na maambukizi ya bakteria, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), shinikizo la damu na mama kutopata lishe bora wakati wa ujauzito” ameongeza Dkt. Lucy.

Kwa upande wake mama mwenye mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati, Bi. Scholastica Mlingi amesema alipata mtoto huyo mwaka 2016 ambapo alijifungua ujauzito ukiwa na miezi saba na kufanikiwa kupata mtoto wa kike mwenye uzito wa Kg. 1 ambaye kwa sasa ana miaka 8.

Bi. Scholastica ameishauri jamii kuachana na dhana potofu mama anapopata mtoto kabla ya wakati na kutoa ushirikiano kwake na familia kwa ujumla kwakuwa malezi ya mtoto huyo yanahitaji ushirikino na mshikamano miongoni mwa jamii.

Siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati huadhiminishwa Novemba, 17 kila mwaka ambapo lengo lake ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto, kujadiliana maendeleo na kubadilishana uzoefu kuhusu malezi ya watoto hao.

Post a Comment

0 Comments