Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Ingawa mabadiliko ya tabianchi yanatajwa kuuathiri ulimwengu kwa ujumla wake, kiuhalisia Bara la Afrika ndilo linalojikuta katika hali mbaya zaidi.
Licha ya mchango mdogo wa Afrika katika uzalishaji wa hewa ya ukaa, bara hilo hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, linakumbwa na atari zaidi ikiwemo joto kali, mifumo isiyotabirika ya hali ya hewa na majanga ya asili.
Pamoja na uhalisia huo, kiwango cha fedha za kuwezesha kuhimili mabadiliko ya tabanchi kinachozifikia jamii zinazokumbwa na misukosuko hiyo ni chini ya asilimia 10.
Kwa miongo kadhaa, mijadala ya kimataifa kuhusu hatua za kuleta afua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi imetawaliwa na sera zisizoakisi uhalisia wa jamii zinazoathirika zaidi.
Hata hivyo, kuna matumaini mapya, baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Urekebishaji wa Tabianchi Unaotokana na Jamii (Locally-Led Adaptation - LLA).
Mpango huo, unakuja kama mbadala utakaoshughulikia changamoto zinazoikumba Afrika na kuziwezesha jamii zilizopo kwenye athari zaidi.
Pamoja na hatua hizo je, dunia iko tayari kukabidhi rungu la kukabili mabadiliko ya tabianchi kwa wale wanaokabiliana na nayo kila siku?
Kwa nini LLA ni muhimu
LLA inalenga kuzipa nguvu jamii kubuni na kutafuta mbinu zitakazotoa afua na suluhu ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazokidhi mahitaji yao mahsusi.
Dhana hii inajengwa juu ya misingi wa ugawaji wa mamlaka ya maamuzi, uwazi, na uwekezaji wa ndani.
Shirika la Kimataifa la Mazingira na Maendeleo (IIED), mwaka 2020, linaeleza njia hiyo inaweza kuziba pengo la fedha za tabianchi na kushughulikia ukosefu wa usawa wa kimuundo unaowaathiri zaidi wanawake, vijana na makundi mengine yaliyotengwa.
Mathalani, ripoti ya mwaka 2022 kuhusu mwelekeo wa urekebishaji nchini Kenya ilionyesha kamati za tabianchi za ngazi za jamii zilitekeleza miradi 284 ya gharama nafuu, ikihusisha usalama wa maji, misitu ya kilimo, na usimamizi wa mifugo.
Miradi hii inaonyesha jamii zikipewa rasilimali na mamlaka ya maamuzi, zinaweza kuleta mabadiliko chanya.
Changamoto
Pamoja na matumaini hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi (FORUMCC), Sarah Ngoy anaweka wazi kuwa LLA inakabiliwa na changamoto, hasa kwenye suala la fedha.
Kwa mujibu wa Mpango wa Kuongeza Kasi ya Urekebishaji wa Afrika (AAAP), Afrika inahitaji dola bilioni 25 kufikia mwaka 2025 ili kuongeza miradi ya urekebishaji.
Taasisi za Kifedha za Maendeleo ya Kimataifa (DFIs) kwa sasa huchangia sehemu kubwa ya fedha za urekebishaji barani Afrika, zikiwa zimeahidi dola bilioni 6 mwaka 2020.
Hata hivyo, anasema zaidi ya asilimia 53 ya fedha hizi ni mikopo, aghalabu yenye masharti ya kibiashara, hali inayozidi kukandamiza uchumi ambayo tayari upo kwenye changamoto.
Zaidi ya hayo, Sarah anaeleza urasimu katika kupata fedha za kimataifa kama Mfuko wa Tabianchi wa Kijani (GCF) ni kikwazo kingine kikubwa.
“Wenye kuomba fedha lazima waonyeshe mikakati thabiti ya kitaifa ya tabianchi, mifumo thabiti ya utawala, na miradi inayolingana na vigezo vikali ambavyo mataifa mengi ya Afrika yanapata ugumu kuyatimiza,” aliongeza.
Changamoto ngazi ya jamii
Katika ngazi ya jamii, Sarah anasema changamoto ni kubwa zaidi. Jamii mara nyingi hukosa utaalamu wa kiufundi wa kusimamia fedha za tabianchi, huku ukosefu wa teknolojia na taarifa ukiongeza tatizo.
“Ukosefu wa mipango ya uendelevu wa miradi ya urekebishaji pia umesababisha kusitishwa ghafla kwa ufadhili na hivyo kuwaacha wanajamii wakiwa hatarini zaidi kwa janga lijalo,” alibainisha.
Hata hivyo, Sarah anasema kuna matumaini. “Mpango wa Kiufundi wa AAAP (TAP) umelenga kuimarisha uwezo wa ndani wa kupanga na kutekeleza miradi mikubwa ya urekebishaji,” alisema na kuongeza kuwa mpango huo wa Afrika unaonyesha nguvu ya ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za pamoja.
Njia ya mafanikio
Ili LLA ifikie uwezo wake kamili, Sarah anazisisitiza Serikali za Afrika na wadau kuchukua hatua za kijasiri.
Kwa mujibu wake Sarah, Serikali hizo zinapaswa kugawa fedha kwa ngazi za chini ili kuanzisha mifumo inayopeleka rasilimali hizo katika ngazi ya serikali za mitaa, mashirika ya kiraia (CSOs), na mashirika ya kijamii (CBOs).
Hatua nyingine anasema ni kuwekeza katika kujengeana uwezo kwa kujipa jamii ujuzi wa kubuni, kusimamia na kudumisha miradi ya urekebishaji.
“Hii inajumuisha mafunzo kuhusu usimamizi wa fedha na tathmini ya miradi,” alifafanua.
Kwa mujibu wa Sarah, hatua nyingine ni kukuza sera jumuishi ili kuhakikisha miradi ya urekebishaji inazingatia makundi yaliyotengwa, wakiwemo wanawake, vijana na jamii za asili.
Kushirikisha wadau mbalimbali ni pendekezo lingine la Sarah ili LLA ifanikiwe, akisisitiza ushirikiano huo unapaswa kuwa kati ya serikali, viongozi wa jadi, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.
Afrika Mashariki ni kielelezo sahihi
Sarah anaeleza Afrika Mashariki inaonyesha mfano mzuri kwa bara hilo. Nchini Kenya, Serikali imeshirikiana na Benki ya Dunia, Denmark, na Sweden kutafsiri sera za tabianchi kuwa hatua za vitendo za ngazi za chini.
“Vivyo hivyo, kamati za tabianchi nchini Tanzania zimeonyesha uwezo wa urekebishaji unaoendeshwa na jamii kupitia miradi midogo lakini yenye matokeo makubwa,” anasema.
Kwa mujibu Sarah, mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano. Hata hivyo, kufanikisha miradi mikubwa kama hiyo kunahitaji mabadiliko ya mitazamo kutoka kuiona jamii kama wapokeaji wa msaada hadi kuwahusisha kama mawakala wa mabadiliko.
Malengo ya Dunia
Profesa Amos Majule wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema LLA si tu kipaumbele cha Afrika bali pia kinahusiana na mifumo ya kimataifa kama Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Kwa mfano, SDG 13 linahimiza hatua za haraka za tabianchi, huku SDG 5 likisisitiza usawa wa kijinsia kipengele muhimu cha urekebishaji wenye ufanisi,” anasema.
Kwa mujibu wa Profesa Amos, miradi inayoshughulikia maji safi (SDG 6) na nishati safi (SDG 7) inaonyesha uhusiano wa karibu kati ya tabianchi na maendeleo.
Hatua za kuchukua
Profesa Amos anasisitiza hali ya Afrika dhidi ya mabadiliko ya tabianchi haiepukiki, kadhalika kurejesha uimara wake, hakupingiki pia.
“LLA ni njia sio tu ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi bali pia kujenga jamii imara zenye kujitegemea,” anasema.
“Lazima tushirikiane Serikali, wafadhili wa kimataifa, na wadau wa ndani, kwani saa inakwenda mbio. Kadri majanga ya tabianchi yanavyozidi kuwa makali, haja ya kuchukua hatua haraka inaongezeka zaidi,” anaongeza.
0 Comments