Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YAITAKA PPPC KUTANUA WIGO WA MIRADI YA UBIA KWA UFANISI ZAIDI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Justine Nyamoga imekitaka Kituo Cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) kutanua wigo wa kutekeleza miradi hiyo ili kufanikisha miradi mingi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa leo Novemba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam, wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo Kamati hiyo juu ya Majukumu ya Kituo Cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

Aidha Kamati hiyo imeipongeza PPPC kwa kuweza kuwajengea uwezo Kamati hiyo na kuweza kuelewa mambo mbalimbali ya kisheria ambayo yanatekelezwa na Kituo hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila amesema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa kuzingatia umuhimu wa teknolojia za kisasa na rasilimali fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini hali itakayosaidia kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati.

Katika Semina hiyo mambo ambayo yamejadiliwa ni pamoja umuhimu wa kutumia PPP katika utekelezaji wa Mipango ya Taifa ya Maendeleo ya nchi, muundo wa kisheria na Kitaasisi katika utekelezaji wa program ya PPP Tanzania.

Mambo mengine ambayo yamejadiliwa ni pamoja na dhana ya PPP na Orodha ya Miradi ya PPP iliyoandaliwa chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Post a Comment

0 Comments