▪️Yatakiwa kuchangamkia fursa mpya za usafirishaji
▪️Yatakiwa kuhakikisha mifumo yake ya utendaji inasomana
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amelitaka Shirika la Posta Tanzania kuongeza ufanisi na ubunifu katika utendaji wake ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi zinazokidgi matarajio yao.
Ameyasema hayo leo tarehe 07 Oktoba, 2024 wakati alipofanya ziara yake yenye lengo la kufahamu utendaji wa Posta katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Silaa ameitaka Posta kuboresha huduma zake kidijitali ili kuendana na mkakati wa Serikali wa Tanzania ya Kidijitali chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kufanya Tanzania ya kidijitali.
Mhe. Waziri ametumia nafasi hiyo kulisisitiza Shirika la Posta kuchangamkia kila fursa mpya za usafirishaji wa bidhaa, mazao, vitu vya thamani na huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Shirika la Posta katika kuendeleza mabadiliko ya Posta kidijitali.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Ya Shirika la Posta Tanzania Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi ameahidi kuwa, Uongozi wa Bodi uko tayari kusimamia mageuzi ya uendeshaji ndani ya Shirika ili kukidhi matarajio ya wateja na wadau wa Posta.
Kwa upande wake Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo ameelezea mpango mkakati wenye vipaumbele vya Shirika vinavyolenga kufanya mageuzi ya Posta ya Kidijitali ili kukidhi mahitaji ya wateja hasa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya Teknolojia.
0 Comments