Ticker

6/recent/ticker-posts

WATEJA WA NHIF WARIDHISHWA NA HUDUMA ZA AFYA, WAOMBA MABORESHO VITUO VYA HUDUMA NA USAJILI.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) unajivunia kuwa na watoa huduma bora za Afya kama sehemu ya wadau muhimu katika kufikia azma ya Bima ya Afya kwa wote na kutimiza malengo ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha uwepo wa huduma bora za matibabu nchini.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Tanga Evance Nyangasi ameyasema hayo katika maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ambapo walitembelea baadhi ya vituo vya Umma na Binafsi vilivyosajiliwa kutoa huduma za afya kwa wanufaika wa Mfuko huo.

Amesema wameamua kuwatembelea wanachama wao katika vituo hivyo ili kupata mrejesho wa huduma za matibabu zinazotolewa na Mfuko, hali ya utoaji wa huduma, kusikiliza kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata maoni ambayo menejimenti ya Mfuko watakwenda kuzifanyia maboresho na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu na kuongeza ari ya utoaji huduma bora kwa wateja wa Mfuko.

"Kama tunavyoelewa lengo na shabaha ya Mfuko ni kutoa huduma bora zaidi na kukidhi matarajio zaidi ya wanachama wetu, kituo hiki cha Siha ni miongoni mwa vituo zaidi ya 450 vilivyosajiliwa kutoa huduma za matibabu kwa Mkoa wa Tanga,

"Tumepeana mrejesho wa huduma na wahudumu wa hapa lakini pia tumeendelea kutoa elimu juu ya huduma bora kwa mteja, tunaelekea kwenye Bima ya Afya kwa wote ambayo lengo la serikali ni kuona kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo na ukwamo wa fedha,

"Na ndiyo maana imetafsiriwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vya serikali nchini nzima vinakuwa na huduma toshelezi lakini pia kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuweka miundombinu mizuri ya afya nchini", amesema.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha Siha Polyclinic Dkt. Kasanga Bashir amesema katika maadhimisho hayo wanaendelea kutoa huduma kwa makundi mbalimbali wenye Bima na wasiokuwa nazo.

"Lakini kundi kubwa la wagonjwa ambao tumewahudumia kwa muda wote ni wateja waliopo chini ya NHIF, niushukuru sana Mfuko huu kwa ushirikiano wao wa kutukutanisha na wateja lakini pia kutusimamia katika mazoezi mbalimbali kuhakikisha kwamba ushirikiano huu unaenda vizuri", amesema.

Dkt. Bashir amebainisha kwamba kufuatia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na serikali katika upatikanaji wa huduma za NHIF kumeleta muitikio mkubwa kwa wananchi jambo ambalo hata wateja wameongezeka kituoni hapo.

"Ikumbukwe kwamba mapema mwaka huu kulikuwa na mabadiliko kidogo wa huduma za NHIF lakini kwa sasa tunashukuru mabadiliko makubwa ambayo yameendelea kufanyika, huduma zinarejea kama kawaida na tunaendelea kupata wateja zaidi wa Mfuko", amebainisha.

Baadhi ya wananchi wanaopata matibabu kupitia Bima ya Afya wamesema huduma zinaridhisha lakini wanaomba kwenye vituo kuwepo na huduma zaidi ambazo hazipatokani huku wakisieitiza uharakishwaji wa usajili pindi mteja anapoanza kujiunga na mfuko huo.

"Tunafurahia huduma za Bima ya Afya lakini tunaombe warekehishe baadhi ya maeneo kama vile una tatizo la macho, unafika kwenye kituo unaambiwa hakuna miwani, hivyo inakupasa utafute tena kituo chenye huduma hiyo, ni gharama nyingine unatumia kutoka kituo kimoka kwenda kingine" amesema Methew Mhando.

Jamal Zuber naye amesema, "wakati wa kujisajili wanatumia muda mrefu hadi mtu kupata huduma, tunaomba warekehishe eneo hilo kuharakisha muda kusajili ili wateja wao wapate huduma mapema, vinginevyo huduma ni nzuri na tunazifurahia".

Post a Comment

0 Comments