Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI ZAIDI YA 15,000 WA KATA YA MAKURO KUPATA MAWASILIANO YA SIMU


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry Silaa (Mb) amesema, wananchi takriban 15,613 wa Kata ya Makuro na maeneo ya jirani wataanza kupata huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika kufuatia kukamilika kwa mnara uliojengwa na kampuni ya Airtel kwa ruzuku inatolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kiasi cha shilingi milioni 115.

Waziri Silaa ameyasema hayo, wakati wa uzinduzi wa mnara huo uliojengwa katika kijiji cha Mikuyu, Kata ya Makuro wilaya ya Singida Mkoani Singida, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Singida.

Akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema, awali mnara huo ulikuwa unatoa huduma kwa teknolojia ya 2G pekee ambayo huwezesha watumiaji kuwasiliana kwa kupiga simu za sauti na kutuma ujumbe mfupi yaani SMS tu, lakini kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2024 mnara huo uliongezewa teknolojia ya 3G na 4G ili kuwezesha matumizi ya huduma za mtandao wa intaneti kupitia simu na vifaa vingine.

Aidha, Mhandisi Mwasalyanda ameongeza kuwa, kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), ambao una jumla ya minara 758 inayojengwa katika kata 713 nchini, Mkoa wa Singida una jumla ya minara 33 inayojengwa katika wilaya za Ikungi, Iramba, Manyoni, Mkalama na Singida.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, ametoa wito kwa wananchi kuutunza mnara huo kwa kuwa kuongezwa teknolojia ya 3G na 4G kutafungua fursa mbalimbali kwa wananchi wa Kata hiyo na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mnara huu utahudumia vijiji vya Mikuyu, Mwalala, Matumbo, Mkenge na Makuro. Aidha utahudumia pia wananchi wa vijiji vya jirani vya Sekotoure, Msimihi na Mjughuda.

Post a Comment

0 Comments