Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAHARAKATI WATAKA MIFUMO YA ELIMU IBORESHWE KUPUNGUZA WATOTO KUKATISHA MASOMO

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wamewasilisha ombi kwa serikali kuhusu kuboresha mifumo ya elimu ili kukabiliana na changamoto ya watoto wanaokatiza masomo. 

Katika semina iliyofanyika leo, Oktoba 2, 2024 Jijini Dar es Salaam, , Mwanaharakati wa Jinsia, Kennedy Anjelita, alisisitiza umuhimu wa kubadilisha mfumo wa elimu ili uwe rafiki kwa kila mwanafunzi, akiongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaoshindwa kumaliza masomo yao.

Anjelita amesema kupitia semina hiyo wamesisitiza kurudishwa kwa elimu ya stadi za kazi shuleni, akisema kuwa inaweza kuwa njia ya kusaidia wanafunzi kujipatia kipato na kuleta manufaa katika shule, ikiwemo kusaidia na masuala ya chakula badala ya kutegemea michango ya wazazi. 

Pamoja na hayo Angelita alipendekeza pia uundaji wa utaratibu wa kukutana kati ya wazazi, walimu, na wanafunzi ili kujadili matatizo yanayowakabili watoto wanaokatisha masomo.

Aidha, Anjelita amesema wameshauri kuhusu adhabu zinazotolewa shuleni, akitaka zirekebishwe ili zisihamasishe wanafunzi kuacha shule. 

Vilevile wadau hauo wamesisitiza umuhimu wa sera itakayoshughulikia watoto wanaoacha shule bila sababu, waakipendekeza kwamba wapelekwe katika magereza ya watoto kwa ajili ya kujifunza.

Kwa upande wake Theodosia Stephano ambaye pia ni mdau wa semina za Jinsia na maendeleo, ameeleza kuwa miundombinu ya shule, ikiwemo ukosefu wa madawati na vyoo ni miongoni mwa sababu zinazowafanya watoto kukatisha masomo. 

Amesema kuwa uhaba wa chakula shuleni kutokana na hali duni ya kiuchumi ya wazazi ni sababu nyingine inayowakatisha tamaa watoto.

Theodosia ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu ili iweze kuwasaidia watoto wenye changamoto na kuwapa fursa sawa za elimu kama wenzao.

Post a Comment

0 Comments