Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI 603 MBAGALA KUU WAHITIMU ELIMU YA MSINGI, WAZAZI WATAKIWA KUWALINDA WATOTO

Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI 603 katika Shule ya Msingi Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam wamehitimu elimu ya msingi huku ujumbe mkubwa ukiwataka wanafunzi hao kutambua safari ya kıelimu ndio imeanza hivyo wajiandae na masomo ya Sekondari kwani Serikali imetoa fursa ya elimu bure.

Hata hivyo katika risala mbalimbali ambazo zimetolewa katika Sherehe za Mahafali ya 49 katika shule hiyo iliyoanza mwaka 1975 zimezungumzia umuhimu wa wazazi kushirikiana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na maadili sambamba na kuwalinda shidi ya vitendo vya unyanyasaji kijinsia.

Mahafali ya wanafunzi hao ambao wamehitimu elimu ya msingi yamefanyika Oktoba 1,2024 na Mgeni rasmi katika mafahali hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Han’s worldwide Services Ltd Hassan Dinya amewapongeza walimu na wazazi kwa kufanikisha safari ya kıelimu ya wanafunzi hao na sasa wanajiandaa kuingia hatua ya pili ya masomo ya Sekondari.

“Tumekutana hapa kwa ajili ya kusherehekea mahafali ya 49 ya shule ya msingi Mbagala kuu ambapo Wanafunzi 603 wamehitimu elimu ya msingi.Katika historia ya shule hii ilianza mwaka 1975 hivyo ni shule kongwe na pia imetoa vipaji vingi.Hata hivyo wakati wanafunzi wanatoa maigizo wametoa ujumbe kwa wazazi na walezi kuwaangalia watoto katika malezi na kuongeza nguvu zaidi katika kuwalinda watoto wa kiume

Kutokana na ujumbe huo Dinya amesema ni kweli hivi sasa kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zinamkuta mtoto wa kiume zikiwemo za unyanyasaji kijinsia na hivyo kusababisha kukatisha ndoto zao ,hivyo wanafunzi wametukumbusha tuwalinde kwa nguvu zote watoto wote

Hivyo ametoa mwito kwa wazazi waangalie watoto wa jinsia zote lakini pia wanapopeleka watoto shule wasiwaachie walimu peke yake katika malezi bali ni jukumu la pande zote mbili kwa lengo la kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya matendo ya unyanyasaji kijinsia lakini kuwajenga kimaadili.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mbagala Kuu Juliana Lubuva amesema wakati leo wanasherehekea mahafali ya 49 shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 4676 na waliohitimu mwaka huu ni wanafunzi 603 imeendelea kukua kwa kasi sambamba na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

“Ukiangalia historia ya shule imeanza mwaka 1975 ikiwa na wanafunzi 80 hivyo tumeendelea kukua kwa kasi na wakati imeanza ilikuwa na vyumba viwili na sasa kuna vyumba 35 na madarasa hayo yameongezeka hasa kutokana na juhudi binafsi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwani ameendelea kuijali shule yetu.

“Tangu mwaka 2021 mpaka sasa tumeshajenga madarasa tisa yakiwemo madarasa matano yaliyojengwa mwaka 2023,hivyo tunamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuijali shule yetu.Pamoja na mafanikio tuliyonayo lakini shule yetu ni kongwe hivyo tunahitaji maboresho makubwa ya madarasa,hivyo tunaiomba serikali itusaidie kwa kutenga fedha.”

Kuhusu taaluma Mwalimu Lubuva amesema anawapongeza walimu,wazazi na viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na wanafunzi kufanikisha kuongeza ufaulu kwani huko nyuma ilikuwa inakuwa katika nafasi za mwisho mwisho lakini kuanzia mwaka 2021 ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 75 mpaka asilimia 98

Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu Mahanya Mahanya amesema shule hiyo imebeba jina la kata yao na ni shule kongwe huku akitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi kutambua safari ndio imeanza.

“Bahati nzuri Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fursa ya elimu bure kwa hiyo tunahakika watoto hao watajiinga na masomo ya Sekondari ili waweze kutimiza ndoto zao na hatimaye kulitumikia Taifa.”

Pia amesema anatambua kuwa kumekuwa na changamoto ya kimaadili hata katika Kata ya Mbagala Kuu lakini wanaishukuru Serikali kwani kupitia Jeshi la Polisi wameendelea kushirikiana na viongozi pamoja na wazazi kusimamia maadili huku akitoa rai kwa wazazi kutambua jukumu la malezi sio la walimu peke yao bali ni jukumu la pande zote.

Post a Comment

0 Comments