Ticker

6/recent/ticker-posts

Tunaendelea kuwekeza kwenye TEHAMA - Mhe. Silaa.

Na Grace Semfuko, Maelezo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa, amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), na kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi pamoja na kujenga uwezo kwa watanzania, lengo likiwa ni kuifanyia Tanzania kuwa sehemu ya mabadiliko ya teknolojia Duniani.

Mhe. Silaa ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2024 wakati akifungua kongamano la nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Tanzania, linaloendelea Jijini Dar es Salaam.

Amesema Wizara anayoiongoza pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kusimamia sera ya TEHAMA 2016 ambayo inalenga kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kasi kubwa katika TEHAMA ambayo ndio nguzo kuu ya kufikia Uchumi wa Kidijitali Duniani, Dunia hivi sasa ipo katika kipindi cha Mapinduzi ya Nne, Tano na Sita ya viwanda ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji kwa kiasi kikubwa inakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA." Amesema Mhe. Silaa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla amesema kongamano hilo la nane limekuwa na sura ya kimataifa kutokana uwakilishi mkubwa wa mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoziwalilisha nchi zao nchini, ambapo pia Tanzania imekuwa nchi ya kwanza wenyeji katika kutoa tuzo ya kimataifa ya akili mnemba na roboti, iliyoandaliwa na umoja wa Afrika.

"Umoja huu umebuni tuzo ya akili mnemba na robot kwa hiyo Tanzania imekuwa nchi ya kwanza wenyeji kutoa tuzo hizo ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" amesema Bw. Abdulla.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, amesema kongamano hilo la mwaka huu limelenga zaidi kujadili masuala ya akili mnemba na roboti.

Post a Comment

0 Comments