Ticker

6/recent/ticker-posts

TRA Yaongeza Ushirikiano na Mabenki ili Kuboresha Ufanisi wa Ukusanyaji Kodi

Na. Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kukuza ushirikiano na wadau mbalimbali wa kodi ambapo leo kwa kushirikina na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekutana na Watendaji Wakuu wa Mabenki na Wakuu wa Taasisi za Kifedha nchini kwa lengo la kujadili masuala ya kikodi.

Akizungumza wakati wa kikao kilichowakutanisha viongozi hao kilichofanyika katika ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Yusuph Mwenda, amesema kikao hicho pia ni njia mojawapo ya kujadili namna bora ya kukuza biashara kwa taasisi za kifedha na kurahisisha upatikanji wa kodi ambayo ndio msingi wa maendeleo ya Taifa.

Kamishna Mkuu Mwenda ameeleza kuwa, kwa sasa TRA imepunguza kutumia Hati ya Uwakala (Agency Notice) na kufafanua kuwa, hati hiyo hutumiwa kama njia ya mwisho baada ya mlipakodi kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kulipa kodi kwa wakati na hiari.

“Kabla ya kutumia hati ya uwakala, TRA humuandikia mlipakodi Hati ya Madai (Demand Notice) na asipotimiza wajibu wake huandikiwa barua ya kumkumbusha na kumtaka alipe kodi anayodaiwa au afike ofisini kwa majadiliano. Mlipakodi akishindwa hatua hizo, ndipo hati ya uwakala hutumwa benki ili kuzuia akaunti ya mlipakodi.” Alifafanua Kamishna Mkuu Mwenda.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba alisema mabenki ni miongoni mwa taasisi zinazolipa kodi kubwa na pia yanatumika kama mawakala wa kukusanya kodi na kutunza fedha za walipakodi, hivyo, kukutana na taasisi hizo ni jambo la muhimu sana katika kuboresha mazingira ya ukusanyaji kodi nchini.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw. Theobald Sabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) alisema kwamba, wamefurahi kukutanishwa na TRA na BoT kujadili masuala ya kodi ili kuleta urahisi katika suala zima la ukusanyaji mapato nchini.

“Ninampongeza Kamishna Mkuu wa TRA kwa hatua hii kubwa ambayo anaendelea kuchukua ya kukaa na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwasikiliza na kujadili namna bora ya kukusanya mapato lakini pia kuondoa changamoto zinazokwamisha walipakodi kulipa kodi kwa wakati.

Wateja wetu watapata morali ya kuendelea kufanya biashara na kuweka fedha zao kwenye mabenki ambayo ni mifumo rasmi ya kibiashara,” alieleza Mwenyekiti wa TBA Bw. Theobald Sabi.

Post a Comment

0 Comments