Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KWENYE MAONESHO TIMEXPO

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu ya viwango kwa wafanyabiashara,wenye viwanda na wananchi kwa ujumla katika Maonesho ya Wazalishaji wa Bidhaa za Viwanda (TIMEXPO) yanayofanyika katika viwanja vya sabasaba Jjijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 01,2024 Jijini Dar es salaam kwenye banda lao, Afisa Masoko Mwandamizi (TBS) Rhoda Mayugu amesema watumiaji wa bidhaa wanatakiwa kukagua bidhaa  pale wanapohitaji kununua ikiwa kama zinakidhi matakwa ya sheria za viwango ili kuepuka gharama au hasara inayoweza kujitokeza kwa kutumia bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wake.

"Watumiaji wa bidhaa wanatakiwa kuhakikisha kwamba bidhaa wanazotumia hazijakwisha muda wa matumizi ili waendelee kutumia bidhaa ambazo ni bora. "Amesema.

Amesema kuwa watu wanapotumia bidhaa ambazo zimethibitishwa ubora wake na TBS,watakuwa wamejiweka eneo salama zaidi kiuchumi pamoja na kiafya.

Aidha Rhoda ametoa wito kwa wajasiriamali wadogo na wakati ambao hawajathibisha bidhaa zao kujitokeza ili kupata alama ya ubora bila malipo ambapo itawanufaisha kwa kuongeza wigo wa kufanya biashara ndani na nje ya nchi. 

Pamoja na hayo Rhoda amewaomba watumiaji wa bidhaa kutoa taarifa endapo watakutana na bidhaa zisizo na viwango au zilizoisha muda wa matumizi kwa lengo la kudhibiti bidhaa hizo kutumika.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Kampuni ya Himo Tanners and planters ltd, Aman Nyange amesema alama ya ubora ya TBS imemtanulia wigo mpana wa kutangaza bidhaa zake ndani na nje ya nchi.

Nyange amewashauri wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa nchini kuwatembelea TBS ili waweze kupata elimu ya ubora wa bidhaa na kuweza kuona umuhimu wa bidhaa zao kuthibitishwa na kupewa alama ya ubora.

Post a Comment

0 Comments