Ticker

6/recent/ticker-posts

RC TANGA AKUMBUSHA WALIOKUWA VIONGOZI SERIKALI ZA MITAA KUTII AGIZO.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Burian, amewahadharisha wananchi mkoani Tanga wasifanye makubaliano yoyote ya kimkataba wa ununuzi wa ardhi na wenyeviti wa mitaa ambao wamemaliza muda wao leo.(kesho).

Dkt Burian amesema kwa mujibu wa Sheria namba 21 ya tangazo la serikali 572 kanuni ya 22 na 571, 573 na 574 ya Julai 12, 2024 kuhusu ukomo wa viongozi hao, hawaruhisiwi kufanya jambo lolote la kimkataba wa kisheria.


Aidha amesema ukomo wao umefikia ukomo leo ambao ni saba kabla ya wagombea wa nafasi hizo hawajachukua fomu ya kugombea katika vyama vyao vya siasa zoezi litakalofanyika ifikapo Oktoba 26 mwaka huu.


"Ili kutoa fursa ya demokrasi na uhuru na kila raia ana sifa ya kugombea hivyo inabidi iongozi hao muda wao ukome, kwamaana shughuli zao walizokuwa wakizifanya zitashikwa na watendaji kwenye maeneo yao" amefafanua..


Dkt Burian amewataka viongozi hao kutii takwa hilo la kisheria ya mamlaka yao na wasijihusishe kwa namna yoyote ile ya utendaji na majukumu waliokuwa wakitekeleza kwasababu sasa muda wao umekwisha na kufanya hivyo ni kosa na endapo watafanya mkoa utawachukulia hatua.


Amesema Mkoa unao wajibu wa kulielekeza jambo hilo na kulishusha katika ngazi za Wilaya ili viongozi hao wajue ukomo wao baada ya Wizara husika kutoa maelekezo.


"Maamuzi yoyote watakayofanya leo ama wameyafanya jana au huko nyuma ambayo yanakinzana na serikali ikiwemo kuingia mkataba isiyokuwa ya kihalali kugawa maeneo ya utawala wao wakishirikiana na wajumbe wao wajue tutasitisha maamuzi yao na tutawachukulia hatua za kisheria", amesema.


Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa amekutana na kufanya mkutano na viongozi wa dini kupitia baraza lao la Amani la Mkoa huo kuhamasiashana umuhimu wa kuwahamasisha waumini wao waende wakajiandikishe.


Amesema viongozi wa dini watumie majukwaa yao ya kukutana na waumini wawahamishe waende kujiandikisha lakini pia Novemba 27 wajitokeze kwenda kupiga kura kuchagua viongozi wao.


Vile vile amesema zoezi la andikishaji lina umuhimu wa pekee kwakuwa linachagua viongozi wazuri ambao wataweza kusimamia na kuzima migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.


Mwenyekiti wa baraza la Amani la viongozi wa dini mkoani Tanga, Sheikh Jumaa Luwuchu amesema viongozi wa dini siku zote wapo pamoja na serikali kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo na kudumisha Amani, hivyo wanao wajibu wa kuwahamasisha waumini wao waende wakajiandikishe.


Mratibu wa zoezi la uandikishaji mkoani Tanga Sebastian Masanja amesema zoezi la kujiandikisha kwa mwananchi halichukui muda mrefu zaidi ya dakika mbili hivyo amewataka wananchi kutumia siku zilizobaki kwenda kujiandikisha Ili wapate haki yao ya kuchagua viongozi wazuri kwa ajili ya maendeleo yao.

Post a Comment

0 Comments