Ticker

6/recent/ticker-posts

NEMC YAWAPA ELIMU KIKUNDI CHA WANAWAKE NA SAMIA - DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha semina ya siku moja ya elimu ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira kwa kikundi cha Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma.

Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa NEMC Makao Makuu Dodoma na kuhusisha viongozi takribani 25 wa kikundi cha Wanawake na Samia kutoka Wilaya saba za Mkoa wa Dodoma.

Akifungua semina hiyo, Meneja wa NEMC Kanda ya Kati (Dodom) Dkt. Caren Kahangwa amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu Utunzaji wa Mazingira na fursa zilizopo katika maeneo ya Urejelezaji wa taka, nishati safi na matumizi ya mifuko mbadala.

Amesema elimu waliyoitoa kwa kikundi hicho itasaidia kuongeza uelewa kwa Wanawake na Samia namna bora ya Utunzaji wa Mazingira ili kupunguza uharibifu, pia ametoa wito kwa kikundi hicho kuziendea fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Mazingira kama biashara ya Hewa Ukaa na Urejelezaji wa taka ngumu, plastiki na taka hatarishi kama vile chuma chakavu.

“Mafunzo tuliyotoa leo tumelenga kuongeza uelewa kwa jamii namna bora ya kutunza Mazingira na pia tupande miti ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa ni pamoja na kutumia nishati safi ya kupikia. Mafunzo haya leo naamini yatawasaidia kuangalia fursa zinazotokana na Mazingira, fursa hizo ni kama kupanda miti ili kuvuna hewa ukaa, utengenezaji wa mifuko mbadala ya karatasi na Urejelezaji wa taka za plastiki, ngumu na taka hatarishi” amesema Dkt. Caren

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Mkoani Dodoma Bi. Fatuma Madidi amepongeza juhudi za Baraza kutoa elimu ya Mazingira kwa jamii. Pia ameahidi kama kiongozi atahakikisha elimu inawafikia wanachama wote na jamii kwa ujumla ili Mazingira yawe salama.

Naye Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma NEMC Bi. Irene John amesisitiza kuwa elimu hiyo itakuwa endelevu kwa Wanawake na Samia katika Mikoa mingine Nchini Tanzania na kutoa wito kwa Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma kuweka nguvu zao kwenye Utunzaji wa Mazingira.

Mada zilizotolewa ni pamoja Maana ya Mazingira na faida za kutunza Mazingira, Katazo la Mifuko ya Plastiki, Urejelezaji wa Taka ngumu, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Mada zimetolewa na Meneja wa NEMC Dodoma Dkt. Careen Kahangwa pamoja na Afisa Mazingira Mkuu Bw. Ahmad Hassan.

Post a Comment

0 Comments