Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI PINDA AITAKA NHC KUJENGA NYUMBA ZENYE UHITAJI MIJINI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (kushoto) akimkabidhi hati milki ya Ardhi Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) mkoa wa Arusha Bw. Lorivii Jeremiah Long’idu (Kulia) wakati wa hafla ya kukabidhi hati kwa wananchi walionunua viwanja kupitia mradi wa Safari City Arusha tarehe 24 Oktoba 2024.

********************

Na Mwandishi Wetu, Arusha


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujenga nyumba zenye uhitaji katika maeneo ya mijini.

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 24 Oktoba 2024 jijini Arusha wakati akikabidhi hati milki za ardhi kwa wananchi walionunua viwanja kupitia Mradi wa Safari City unaotekelezwa na Shirila la Nyumba la Taifa (NHC).

Jumla ya hati 240 zimeshagawiwa kwa wanunuzi wa viwanja katika mradi huo ambapo katika tukio hilo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amekabidhi hati milki 30 kati ya 81 zilizoandaliwa.

‘’Vijumba vingine vilivyopo kati kati ya mji kwa kweli ni kama vile vya urithi, havina sura ya Tanzania ya sasa, muende mkaweze upya ili tupate thamani inayofanana na uhalisia.

Amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutouza nyumba zilizopo kati kati ya miji na badala yake wazibomoe na kujenga upya kulingana na uhitaji wa maeneo husika.

‘’Ukiweka hata ukumbi utapata wapangaji wengi, ukijenga mahoteli watu watakuja kupanga na kuendesha shughuli zao’’. Amesema mhe. Pinda

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Arusha Bw. Benit Masika amesema, shirika lake hadi sasa limeweza kuuza jumla ya viwanja 1,026 ambapo kati ya hivyo viwanja 350 wateja wake wamemaliza malipo kwa asilimia 100.

‘’Naomba ieleweke kwamba NHC imeazimia kuuza viwanja kwenye mradi huu wa Safari City kwa malengo ya kutoa fursa ya uendelezaji kwa wananchi na wadau’’. Amesema Bw. Masika.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa NHC mkoa wa Arusha, mradi wa Safari City tayari umefikiwa na huduma wezeshi kwa wateja kama vile maji, umene pamoja na miundombinu ya barabara aliyoieleza kuwa, imekuwa ikiendelezwa na serikali ili kuwawezesha walionunua maeneo kuendeleza maeneo yao.

‘’ Shirika limetenga viwanja 1,601 kwa ajili ya kuviuza na viwanja 313 shirika limehifadhi kwa ajili ya uendelezaji wa baadaye’’. Amesema Bw. Masika

Baadhi ya wanunuzi wa viwanja kupitia mradi huo wa Safari City wamefurahi na kuishukuru serikali kwa kuwakabidhiwa hati milki za ardhi katika eneo hilo walilolielezwa kuwa limepangiliwa vizuri na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) mkoa wa Arusha Bw. Lorivii Jeremiah Long’idu ambaye Taasisi yake ni moja waliokabidhiwa hati kupitia mradi wa Safari City amesema, ofisi yake baada ya kukabidhiwa hati milki, sasa itaanza ujenzi wa ofisi ya kanda ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya mkoa.

‘’Jengo hili litakapokamilika litakuwa likitoa huduma katika kanda ya kaskazini’’. Amesema Long’idu

Mradi wa Safari City ulioandaliwa eneo la ekari 587 katika mpango kabambe ulioandaliwa mwaka 2014 upo eneo la Burka Mateves ndani ya jiji la Arusha. Mradi huo una jumla ya viwanja 1913 kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba za makazi, majengo ya biashara, huduma za jamii kama vile shule, vyuo, hospitali, sehemu za ibada, sehemu za michezo, kupumzikia na maeneo ya usalama wa miji kama vituo vya polisi, zimamoto na maeneo ya viwanda vido vidogo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wananchi aliowakabidhi hati kupitia mradi wa Sfari City unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 24 Oktoba 2024.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Arusha Bw. Benit Masika akizungumza wakati wa hafla ya utoaji hati milki za ardhi kwa wananchi walionunua viwanja kupitia mradi wa Safari City unaotekelezwa na Shirika lake mkoani Arusha tarehe 24 Oktoba 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Post a Comment

0 Comments