Ticker

6/recent/ticker-posts

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI AFANYA MAZUNGUMZO NA MGOMBEA URAIS WA CHAMA CHA FRELIMO

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume ameendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji ambapo tarehe 04 Oktoba, 2024 jijini Maputo amekutana na kufanya mazungumzo na Mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Chapo alimweleza Mhe. Dkt. Karume masuala mbalimbali kuhusu maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 09 Oktoba 2024.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Karume alimshukuru Mhe. Chapo kwa taarifa yake na kumweleza lengo la Misheni anayoiongoza kuwa ni kuangalia uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021 na kuridhiwa na nchi wanachama. Pia alitumia nafasi hiyo kuwatakia wananchi wa Msumbiji uchaguzi mwema wa amani na utulivu.

Wakati wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Karume aliambatana na Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania, Zambia na Malawi, Sekretarieti ya SADC akiwemo Mwenyekiti wa Troika, Prof. Kula Ishmael Theletsane na Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC). Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema.

Mhe. Dkt. Karume kwa nafasi yake ya Mkuu wa Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC ameendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambapo hadi sasa amekutana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji na Kamishna Msidizi wa Jeshi la Polisi la Msumbiji.
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza na Mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo. Mazungumzo yao yamefanyika tarehe 04 Oktoba 2024 jijini Maputo. Uchaguzi wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji utafanyika tarehe 09 Oktoba 2024.
Mazungumzo yakiendelea ambapo Mhe. Chapo amemweleza Mhe. Dkt. Karume kuhusu maandalizi ya uchaguzi ya Chama chake kuelekea uchaguzi tarehe 09 Oktoba 2024
Mhe. Chapo akizungumza
Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania ambao walishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema
Wajumbe wa Troika kutoka Zambia nao wakishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani).
Wajumbe wakishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani).
Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume akiagana na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo baada ya kumaliza mazungumzo yao
Picha ya pamoja

Post a Comment

0 Comments