Ticker

6/recent/ticker-posts

MIAKA 50 YA HIFADHI YA TAIFA KATAVI YAENDA SANJARI NA UZINDUZI WA UJENZI WA NYUMBA 12 ZA MAAFISA NA ASKARI WA UHIFADHI - KATAVI.

Na. Jacob Kasiri - Katavi.

Furaha imetamalaki katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Katavi leo tarehe 29 Oktoba, 2024 wakati wa sherehe hizo baada ya mradi wa kuhifadhi ikolojia ya Hifadhi za Taifa Katavi, Milima Mahale na Ushoroba unaounganisha hifadhi hizi almaarufu KAMACO kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 12 za watumishi zinazotarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita huku zikigharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.6.

Nyumba hizo za kisasa zitakazopunguza changamoto ya makazi kwa maafisa na askari wa hifadhi hii, zimebuniwa na zitajengwa kwa kuendana na mabadiliko ya tabia nchi, kwani ujenzi wake pia utatumia malighafi ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Akiweka jiwe la Msingi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu alisema, “Tunashukuru KAMACO kwa uboreshaji wa makazi kwa maafisa na askari wa hifadhi hii kwani wamekuwa mstari wa mbele kulinda hizi rasilimali. Hivyo niwatake zitakapokamilika mzitunze ili zitumike kwa muda mrefu.”

Aidha, Mhe. Buswelu aliongeza, “Wakati tukisherehekea miaka 50 ya hifadhi yetu tumeona ongezeko kubwa la watalii wa nje na ndani kutembelea hifadhi zetu, Katavi ikiwa ni mojawapo, hivyo niwatake wananchi mnaokaa kandokando ya hifadhi hii kuchangamkia fursa za uwekezaji, kuuza mazao ya chakula kwa wageni ili kujiongezea kipato.”

Akimkaribisha mkuu huyo wa wilaya, Naibu Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA na Mkuu wa Kanda ya Kusini Steria Ndaga alisema, “Ujenzi wa nyumba 12 zitapunguza changamoto ya upungufu wa nyumba unaoikabili hifadhi yetu, hivyo tuwashukuru wadau wetu kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa kuja na hii suluhu”.

“Kama tulivyodokezwa na Mhandisi anayejenga nyumba hizi kuwa zimebuniwa kuendana na mazingira ya joto kama hifadhi yetu ilivyo, hivyo zitakuwa na uwezo wa kuruhusu mzunguko wa hewa, kupunguza joto, kuzuia popo na kuvuna maji ya mvua ili kukabili uhaba wa maji kwa watumishi nyakati za kiangazi”, aliongeza Kamishna Ndaga.

Naye, Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS) Dkt. Ezekiel Dembe wanaotekeleza mradi huo kwa usimamizi wa Wizara ya Maliasili alisema, “Kwa Katavi mradi huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.1 zitakazotumika katika ujenzi wa nyumba 12, Barabara, gereji ya kisasa, ujenzi wa Hanga la ndege, madaraja 4 na ununuzi wa magari.”

Kwa upande wa kukabiliana na uhaba wa maji kwa wanyamapori ndani ya hifadhi hii hususani kipindi cha kiangazi, mradi utajenga mabwawa ili kuondoa tatizo la wanyamapori hao kwenda kutafuta maji vijiji vya jirani na kuleta kero na madhara kwa wananchi aliongeza mkurugezi huyo.

Mradi huu wa kuhifadhi ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Katavi, Milima Mahale na Ushoroba unaoziunganisha hifadhi hizi mbili wa KAMACO pia umejikita katika kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi mbili.

Katika kuboresha maisha ya wananchi hao, mradi umetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.8 ambazo zitatumika katika ujenzi wa Zahanati, madarasa, ofisi za vijiji na kuboresha huduma za maji. Uboresha wa miundombinu hiyo itawafanya wananchi watambue thamani ya uhifadhi katika maeneo yao na wawe na uchungu wanapoona wachache wakizihujumu.

Hata hivyo, miaka mingi Hifadhi za Taifa Tanzania na Shoroba nyingi ambazo ni mapito ya wanyamapori kwa ajili ya kwenda kwenye malisho na maji zimeendelea kuwa ni mhanga wa uvamizi unaofanywa na wananchi wanaokaa kandokando ya hifadhi.

Katika kukabiliana na uvamizi huo, mradi huu wa KAMACO umejipambanua kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi, elimu ya mazingira na kuwajengea wananchi uwezo wa vyanzo vingine vya mapato ili kuondokana na uvamizi wa mara kwa mara wa hifadhi na shoroba ambazo ni mazalia na mapito ya Sokwe.

Mradi huu wa Katavi-Mahale Ecosystem and Corridor Conservation Project (KAMACO) wenye lengo kuimarisha ikolojia na kukuza utalii wa hifadhi hizi 2, unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) chini ya usimamizi TANAPA kwa kushirikiana na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS).

Post a Comment

0 Comments