Ticker

6/recent/ticker-posts

Dkt. Mataragio Apongeza Puma Energy kwa Kuandaa Tuzo kwa Mawakala Wake

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio ameipongeza Puma Energy Tanzania kuandaa Tuzo kwa ajili ya mawakala na washirika wake ili kuwaleta pamoja wafanyakazi na wadau mbalimbali pamoja na kuongeza ufanisi wa kazi katika kuwahudumia watanzania kwa ujumla.

Akizungumza Oktoba 25, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa Tuzo kwa Mawakala wa Puma Energy Tanzania mwaka 2024, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt.James Mataragio amesema utaratibu huo wa kuwakutanisha wadau wake kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu na kujadili muelekeo wa sekta ya nishati nchini.

“Matukio kama haya yanamchango mkubwa na ni afya kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu kwasababu mijadala inayatolewa na mrejesho halısı unaopatikana kutoka kwa walaji wa mwisho wa bidhaa ambao ni wananchi unasaidia sana". Amesema

Amesema Rais Samia amekuwa akifanya kazi kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za nishati za uhakika na gharama nafuu.

"Rais amekuwa akifanya jitihada kubwa kuhakikisha mazingira na miundombinu ya sekta ya nishati inakuwa rafiki na bora kwa uwekezaji wa biashara pamoja na kuwafikia Watanzania wote bila kujali hali za vipato vyao" . Amesema Dkt. Mataragio.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Puma Energy Tanzania Dk.Seleman Majige amesema wamepanga kuanza mchakato wa kuuza gesi ya kwenye magari katika vituo vyao ifikapo mwezi Machi 2024 hivyo wananchi wametakiwa kujiandaa kununua gesi katika vituo vya Puma Energy.

Amesema kuwa soko la gesi ya magari ni kubwa na wananchi wengi wameitikia kwa kubadilisha magari kutoka kwenye kutumia petroli na dizeli kwenda katika mfumo wa gesi.

“Lengo letu ni kupunguza foleni kubwa katika vituo vinavyofanya biashara ya gesi ya magari na tunategemea kwa miaka inayokuja basi tutaenda mpaka mikoani. Niwaombe wananchi muendelee kutuunga mkono lakini na kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kama jinsi ambavyo anasisitiza suala la nishati safi". Amesema

Aidha amesema Puma inayomilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali imekuwa na mkakati mbalimbali na mkakati mmojawapo ni nishati safi ambayo ni matumizi ya gesi.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah akizungumza tuzo hizo amesema kampuni yao inatambua umuhimu wa mawakala na washirika wao katika kufanikisha uendeshaji wenye mafanikio ya kufikia wateja na Watanzania kwa ujumla nchini kote.

“Shughuli hii inafanyika kila mwaka na hii ni mara nne ambapo mbali na hilo tunafahamu kutoa tuzo kwa wakala na wadau wetu ni kutambua mchango wao lakini pia kuimarisha mahusiano , kubadilishana mawazo kuhusiana na mwenendo wa utoaji huduma zetu na mustakabali wa maendeleo ya sekta ya nishati nchini kote".

“Puma Energy Tanzania inajivunia kuwa na mawakala nchi nzima.Pamoja na hayo tutaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha kampuni yetu inaunga mkono jitihada za Serikali za upatikanaji wa huduma na bidhaa bora za nishati safi na tumejidhatiti kutekeleza dhamira ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kufanikisha kampeni ya nishati safi ya kupikia,”amesema Fatma Abdallah.

Ameongeza kuwa Rais Samia ndio kinara katika jitihada hizo ikiwa ni mkakati wa kuwasaidia wananchi wote kuhamia katika nishati safi ili kuepukana na madhara ya kiafya na kimazingira kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.”Kwa pamoja Puma Energy tunaamini mkakati huu utafanikiwa na tayari tuna Puma Gas sokoni.”

Post a Comment

0 Comments