Ticker

6/recent/ticker-posts

DC KUBECHA ATOA AGIZO LA MSAKO VYUMA CHAKAVU BAADA YA MIUNDOMBINU BARABARANI KUIBIWA


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

VIONGOZI wote wa kata, mitaa na vijiji wametakiwa kulinda miundombinu ya aina zote iliyowekwa na serikali kwa matumizi ya wananchi iliyowekwa barabarani na kuufichua mtandao wa wizi ambao inahujumu miundombinu hiyo na kuiuza kwenye vyuma chakavu.

Wito huo umetolewa na Meya wa jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloow katika kikao cha baraza la madiwani ambapo alisema sambamba na hilo pia wanapaswa kulinda na kutunza mazingira ya barabara na mifereji.

'Wakati wa zoezi la sensa,, halmashauri hiyo ilitenga kiasi cha shilingi millioni 402 kutoka fedha za mapato ya ndani kuweka vibao vya post code, lakini wametokea watu wasiokuwa wazalendo, wanaondosha nguzo na vile vibao vya alama za mitaa,

"Lakini pia kumekuwa na uharibifu wa barabara za Kitaifa, pembezoni kuna zile kingo ambazo zina vyuma ndani, watu wanavunja na kwenda kuuza kwenye vyuma chakavu, kwahiyo mkuu wa Wilaya kwa nafasi yako tunaomba vyombo vyako vya ulinzi vitusaidie" amesisitiza.

Hata hivyo amewaomba wananchi kutunza mazingira kwa kulipendezesha jiji kwa kusimamia usafi wa nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na kata zao kwa ujumla lakini pia kwa kila mwenye nyumba afunge taa nje ya nyumba yake kwa ajili ya usalama

Kufuatia hali hiyo, mkuu wa Wilaya ya Tanga Jafari Kubecha ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama kufuatilia maeneo ambayo vyuma chakavu vinauzwa na kufanya upekuzi wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na kuibiwa ili kukomesha mtandao wa wizi wilayani humo.

"Kupitia kikao hiki nimuagize rasmi mkuu wa Polisi Wilaya, kupita na kupekua maeneo yote ambayo vibao miundombinu ya barabarani imeuzwa kwenye vyuma chakavu, na nipate taarifa hiyo ifikapo Novemba 5 ya maeneo yote ambayo taa za barabarani zimeondolea, tunataka kuuondoa huo mtandao,aamini nitapata taarifa nzuri, wezi wapo na wanafahamika, hivyo ni lazima wadhibitiwe ili kulinda miundombinu yetu" amesema.

Pia amevitaka vyama vya siasa kutumia demokrasia bila kupotosha maana yake na kufanya kampeni za kistaarabu kwa kutunza amani na utulivu lakini pia kulindiana heshima baina ya vyama pamoja na wagombea wenyewe.

"Isije ikawa tumefungua uchaguzi iwe ndio chanzo cha kuvuruga amani na utulivu tulionao na kuvuruga maendeleo ambayo tumeyapata, kama serikali tunawaomba sana wanasiasa kutusaidia katika hili, kufanya kampeni safi na siyo za kuvunjiana utu na heshima" amesisitiza

Hata hivyo Kubecha amewataka madiwani hao kutoa ushirikiano katika zoezi la uhamasishaji wananchi kujitokeza kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kwani ndiyo msingi wa maendeleo.

"Tusipokuwa na wenyeviti wazuri shida kubwa mnaoipata ni ninyi madiwani katika ufanisi kwakuwa wale ndiyo kiini na kiunganishi baina yenu na wananchi, kwahiyo niombe mshirikiane kwa pamoja katika kuwahamasisha wananchi wachague viongozi bora" amesema.

Kubecha pia amesisitiza kuhusu miradi ya maendeleo viporo ambayo haijakamilika kwa wakati na kuleta kero kwa wananchi hivyo halmashauri inatakiwa kuweka nguvu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika japo kwa hatua ili kuwaondolea wananchi kero wanazopata.

"Tunakwenda kwenye uchaguzi, kuna miradi singing bado ni kero kwa wananchi, kwahiyo niombe baraza hili tujipande kuweka kuweka nguvu ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kuikamilisha ili tuweze kuwaondolea wananchi kero zilizopo mbele yao" ameongeza.

Sambamba na hayo, halmashauri hiyo imewakabidhi kompyuta mpakato 27 Maofisa Ustawi wa Jamii kila kata kwa lengo la kuboresha huduma na kufanya kazi zao kielektroniki.

Post a Comment

0 Comments