Ticker

6/recent/ticker-posts

BRELA Yaongoza Mkutano wa Wadau Kuimarisha Uwekezaji na Huduma za Kibiashara

SERIKALI imezitaka taasisi za umma, kutofanya kazi kimazoea, badala yake zijiendeshe kibiashara kwa kuleta tija katika ukuaji wa uchumi.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, leo Octaba 25,2024 katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na wadau wake,Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema mkutano huo ni ishara kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na shirikishi ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini.

Kigahe amesema utoaji huduma kibiashara kwa taasisi za umma zitasaidia kukua kwa pato la nchi na kila mwananchi atapata huduma muhimu zikiwemo za kimaendeleo.

Amesema tangu Brela waandae mikutano ya wadau anaamini maboresho yamefanyika ambayo yameongeza ufanisi na ubora wa huduma zake .

“Taasisi zingine za Serikali ambazo bado hazijaanza utaratibu huu, mnatakiwa kuiga mfano huu ni mzuri kwa sababu unawapima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe,”amesema.

Amesema Brela ndio lango la urasimishaji wa biashara ambapo usajili wa makampuni, majina ya biashara,alama za biashara na huduma na leseni zenye sura za Kitaifa na Kimataifa zinafanyika kwao hivyo taasisi hiyo ni muhimu katika ujenzi wa taifa.

Hivyo ameongeza kuwa Brela haiwezi kufanikiwa katika kutekeleza majukumu yake ikiwa pekee yake hivyo inategemea ukaribu wa sekta za umma na sekta binafsi.

“ Mkutano huu ni muhimu kufanyika kwa lengo la kufanya tathmini ya wapi walipotoka na wapi wanaelekea ikizingatiwa nafasi yao katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo,”amesema.

Kigahe amesema amevutiwa na kauli mbiu ya mkutano huo unayosema “Mifumo ya kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini”hivyo ametaka kauli mbiu hiyo ijadiliwe kwa upana kwa sababu mifumo ya kitaasisi inatakiwa kusomana kwa lengo la kutoa huduma zote kwa njia ya mfumo.

“Serikali ilishatoa maelekezo hadi ifikapo Desemba mwaka huu taasisi zote za serikali ziwe na mifumo inayosomana kwa lengo la kuondoa usumbufu na kero wakati wa kuwahudumia wananchi”amesema.

Hata hivyo amesema viongozi na maofisa kutoka nchi ya Burundi,Sudani Kusini,na Kenya wamekuwa wakifika Brela kujifunza namna ya utoaji wa huduma kwa ufasaha na kwa njia ya mifumo.

Kwa upande wake,Afisa Mtendiji Mkuu wa Brela Godfrey Nyaisa amesema mkutano huo una washiriki kutoka sekta za Umma, taasisi na mashirika ya Umma na binafsi,wawekezaji na wafanyabiashara.

Nyaisa amesema mwaka 2015 Brela ilianzisha mfumo wa kwanza wa usajili wa majina ya biashara kwa njia ya mtandao , mfumo huo ulitengenezwa na watumishi wa brela kwa kushirikiana na vijana wengine wa Kitanznaia hiko ni kiashiria tosha kuwa vijana wakiwezeshwa wanaweza

Hata hivyo Nyaisa alisema hivi sasa Brela ina mifumo mizuri na kila wakati wanaendelea kuifanyia maboresho kulingana na mahitaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi Profesa Neema Molel amesema bodi yao imeleta mafanikio ndani ya Brela kwa kufanikisha dhima ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mifumo inasomana.

“Tumeweza kuleta mafanikio ndani ya Brela hadi leo hii tunachangia mfuko wa serikali kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii lakini mifumo ya brela imeweza kusomana na taasisi nyingine za serikali ikiwemo TRA”amesema.

Post a Comment

0 Comments