Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI KANDA YA ZIWA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA YA FANI YA MIPANGO

Wananchi wa Kanda ya Ziwa wamehamasishwa kuchamkua fursa za kusoma kozi za mipango zitolewazo na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichopo Dodoma na Mwanza.

Hamasa hiyo imetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Profesa Provident Dimoso Septemba 08 na 09, 2024 alipozungumza na Wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Simiyu, Geita, Shinyanga,Musoma, na Mwanza kupitia Radio Jembe FM na Inland FM za Mwanza na Sengerema mtawalia lipofanya mahojiano ya moja kwa moja kwa nyakati tofauti katika ziara ya kutembelea vituo vya redio vya Kanda ya Ziwa.

“Ndugu zangu wanakanda ya Ziwa fursa ya vijana wetukupata ujuzi wa fani ya Mipango imesogezwa katika kanda yetu hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha katika Kituo chetu cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza kutuma maombi ya kujiunga na Chuo chetu katika fani mbali mbali za Mipango” Alisema Profesa Dimoso

Aidha, Prof. Dimoso amebainisha kuwa kwa sasa awamu ya pili ya dirisha la udahili kwa programu zote zinazotolewa na Chuo cha Mipango liko wazi hivyo amewakaribisha Wahitimu wa ngazi zote kutuma maombi ya kujiunga kwa njia ya mtandano kupitia oas.irdp.ac.tz.

Pia amesema kuwa Chuo kimeendelea kuongeza baadhi ya program mpya na kuendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya kujifunzia na kufundishia hususani katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza kwa kuanzisha program ya Shahada za Umahiri.

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa mwaka 1979 kwa sheria ya Bunge Namba 8 ya mwaka 1980 kwa madhumuni ya kuimarisha Mfumo wa Madaraka Mikoani ulioanzishwa mwaka 1972 uliojibainisha kwa ugatuaji wa madaraka.

Aidha, Septemba 25, 2011 Chuo kilifungua Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, Mwanza kusogeza karibu huduma za Chuo kwa Wananchi wa Kanda ya Ziwa.

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa kwa madhumuni ya kuboresha shughuli za upangaji mipango ya maendeleo vijijini kwa njia ya kuandaa wataalam wa mipango na kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watendaji na viongozi mbali mbali kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Taifa. Mafunzo haya yanatakiwa yaende sambamba na kufanya utafiti na kutoa ushauri na uelekezi juu ya masuala yahusuyo mipango ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments