Ticker

6/recent/ticker-posts

WANA-DGSS WAJA NA MWAROBAINI WA TATIZO LA MMOMONYOKO WA MAADILI

Ili kuimarisha harakati za uwekezaji katika mifumo ya usalama katika familia ni muhimu kukawepo na ushirikiano katika malezi ya watoto na kwa kufanya hivyo changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii hautakuwepo.

Hayo yamesemwa leo Septemba 04, 2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo hufanyika kila Jumatano ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mabibo jijini Dar es Salaam ambapo mada ya.Mmomonyoko wa Maadili katika familia na Jamii

Akizungumza katika semina hiyo, Mwezeshaji Mpegwa Muhembano amesema kuwa, pasi na ushirikiano katika malezi ya watoto madhara na hasara nyingi hutokea ikiwemo watoto kukosa utii na nidhamu, kutumbukia katika tabia hatarishi za matumizi ya madawa ya kulevya na kufanya ngono wakiwa na umri mdogo.

Amezitaja faida za ushirikiano katika malezi ya watoto kuwa ni pamoja na kupata taarifa za watoto pindi wanapoanza kukiuka maadili na hivyo kuwa na nidhamu katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.

Ameendelea kwa kusema kuwa, kila mzazi au mlezi ana wajibu wa moja kwa moja wa kumfundisha mtoto au watoto stadi za misingi ya usalama na amani ili aweze kujilinda na kuwalinda watoto wengine.

"Kulingana na umri, watoto wanapswa kufundishwa kuepuka tabia ya kuomba omba, kuepuka marafiki wenye tabia hatarishi, kuepuka kucheza michezo hatarishi ikiwemo kamari, kutoaga pindi anapotoka nyumbani kwenda sehemu nyingine, kuwapa mwongozo sahihi wa familia." alisema Bi. Muhembano

Kwa upande wake Stanley Mosha ambaye ni mshiriki wa semina hiyo amesema, kila mzazi au mlezi anapaswa kufahamu kuwa analo jukumu la moja kwa moja la kuhakikisha maadili yanafundishwa na kusimamiwa ngazi ya familia na kwa kufanya hivyo Taifa zima litakuwa na maadili huku akitoa rai kwa mamlaka za sanaa nchini kutilia mkazo eneo la wanamuziki kwa kuhakikisha kwamba nyimbo wanazozitunga hazichangii kwa namna moja au nyingine mmomonyoko wa maadili kwa watoto wamekuwa wakiiga na kuimba nyimbo zao ambazo nyingine zimekuwa hazina maadili.

Naye Hancy Obote akichangia katika semina hiyo amesema, moja ya sababu inayochangia katika mmomonyoko wa maadili katika jamii ni kuingia katika utandawazi pasi na kujiandaa na kupelekea kuacha mila, destruri na tamaduni zetu ambazo nyingine zilikuwa nzuri na zenye tija.

Mshiriki mwingine Veronica Julius ameeleza kuwa, ni vyema jamii kwa ujumla ikishiriki katika kuangalia chanzo na mizizi ya tatizo la mmomonyoko wa maadili katika jamii ili iwe rahisi kupata suluhu ya kudumu.

Bi. Veronica amevitaja miongoni mwa mizizi na vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na udhibiti wa vibanda vya kuoneshea filamu na mpira maarufu vibanda umiza ambavyo vingine hutumika kuonesha picha na video chafu, majengo yasiomalizika ujenzi wake maarufu kama mapagale na baadhi ya mila na desturi ambazo zinamuhamasisha mtoto wa kike kuanza kutekeleza yake aliyofundishwa wakati wa mafunzo yake (unyago).

Katika semina hiyo, wana- GDSS wameweza kushirikishana ufahamu pamoja na kujadili chanzo na mmomonyoko wa maadili pamoja na njia za kuzuia tatizo la mmomonyoko wa maadili.

Kwa upande wa vyanzo vinavvyosababisha mmomonyoko wa maadili, wana-GDSS wamevitaja kuwa ni pamoja na changamoto ya aina za malezi ikiwemo malezi ya kutumia mabavu na kudekeza, watoto kutopatiwa mafundisho ya dini, wazazi kuwa bize na shughuli za utafutaji na kushindwa kupata muda wa kukaa na watoto pamoja na familia, kutokuwa na utaratibu wa kukaa na kuongea na watoto, kutowafundisha na kusisitiza maadili mema kwa watoto, kutokuwa na mtazamo sahihi wa malezi stahiki kwa mtoto, kuingia kwenye utandawazi pasi na kujiandaa, kuiga tamaduni za nje zisizofaa, kuacha mila na desturi nzuri za kwetu pamoja na makundi rika.

Aidha kwa upande nini kifanyike ili kuondokana na tatizo hilo la mmomonyoko wa maadili wamependekeza kuwepo kwa udhibiti wa matumzi ya vifaa vya elektroniki ikiwemo simu janja, TV na kompyuta kwa watoto, kutenga muda wa kukaa na familia, kuwapa watoto malezi bora, kuhuisha na kudumisha mila na desturi nzuri na zenye tija, kuepuka makundi rika, kuacha kuiga tamaduni za nje, kuwapa watoto misingi na mafundisho ya dini, kuwa na kanuni sahihi za malezi bora.

Post a Comment

0 Comments