Ticker

6/recent/ticker-posts

WANA-DGSS WAADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA KIDEMOKRASIA IKIHIMIZA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA MAAMUZI

Septemba 15 ya kila mwaka, wananchi kote duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, siku ambayo inelanga kukumbusha na kuhimiza majukumu na wajibu wa kukuza na kudumisha kanuni za demokrasia duniani kote.

Leo Jumatano Septemba 18, 2024 wadau wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameitumia siku hiyo kama sehemu ya maadhimisho ambapo kwa pamoja wamejadiliana kwa mapana yake kuhusu Demokrasia na Ushiriki wa Wanawake Katika Maamuzi.

Akiwasilisha mada hiyo, mwezeshaji Nelson Munis kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) amesema, ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi ni muhimu kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia na kukuza utawala shirikishi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, ushiriki huo unajumuisha ushiriki wao katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, kuwaruhusu kuathiri sera na mipango inayoathiri maisha na jamii zao.

Vilevile amesema, ushiriki wa wanawake ni muhimu kwa kuwa huleta uzoefu na mitazamo ya kipekee ambayo inaweza kuimarisha mchakato wa kufanya maamuzi na kuzalisha sera pana zaidi na bora.

Ameendelea kwa kusema kuwa, ushiriki wa wanawake katika maamuzi huwezesha wanawake, kuwapa sauti katika masuala yanayohusu maisha yao na kukuza usawa wa kijinsia katika nyanja zote za jamii.

Kuhusu mchango wa ushiriki wa wanaweka katika ukuaji wa uchumi, Munisi amesema "Tafiti zinaonesha kuwa nchi zilizo na viwango vya juu vya usawa wa kijinsia katika kufanya maamuzi zina uzoefu wa ukuaji wa uchumi na maendeleo yenye nguvu."

Kwa upande wake mshiriki wa semina hiyo Kennedy Angeliter amesema, ushiriki wa wanawake katika maamuzi ni jambo muhimu kwa kuwa ni fursa kwao ya kupenyeza ajenda zao ikiwemo kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuimarisha misingi ya haki na usawa katika maeneo yote na kuondoa mifumo na aina zote za ukandamizaji.

Rachel Michael akiwasilisha maoni yake amesema, ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika maaumzi inapaswa elimu ya uongozi inapaswa kutolewa kwa wanawake na kutokukubali kukatishwa tamaa kwa namna yoyote.

Kupitia semina hiyo wana-DGSS kwa pamoja wameanika mikakati ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.

Mikakati hiyo ni pamoja na kutunga sera simamizi za usawa wa kijinsia, kuondoa mifumo dume na kandamizi, uanzishwaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, wanaume kuwaunga mkono wanawake katika michakato ya uchaguzi wa viongozi, uwepo wa wagombea binafsi, kutobagua ushiriki wa wanawake kwenye vikao vya maamuzi, kuhimiza uungwaji mkono kutoka kwa wanaume.

Siku ya Kimataifa ya Demokrasia ina madhumuni kadhaa muhimu ikiwemo ikiwemo kuhimiza raia kujihusisha katika michakato ya kidemokrasia na kuelewa umuhimu wa demokrasia katika kuhakikisha haki za binadamu, uhuru na haki.

Post a Comment

0 Comments