Ticker

6/recent/ticker-posts

Waiomba Tanzania, China kisitisha EACOP

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Green Faith limeiomba Serikali ya Tanzania na China kisitisha ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani Tanga ili kuepusha athari za kimazingira.

Pamoja na Green Faith Taasisi ya Organisation for Community Engagement (ECO), wameungana wakisisitiza kusitishwa kwa mradi huo hadi watakapohakikisha utunzaji wa mazingira unafanyika na kulinda haki za binaadam wanaoishi linakopita bomba hilo.

Mwakilishi wa Green Faith Tanzania, Baraka Lenga alisema hayo hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari masuala ya ukiukwaji wa haki za binaadam na uharibifu wa mazingira unaofanyika kwenye mradi huo.

Alisema mradi huo uliopita kwenye mikoa nane na wilaya 21 za Tanzania unadhulumu haki za wananchi na kuchelewesha maendeleo yao huku ukiharibu uoto wa asili na mazingira.

"Kuna wananchi wamechukuliwa maeneo yao kupisha mradi na walifanyiwa tathimini mwaka 2018/2019 malipo ya tathimini ile wameyapata mwaka huu 2024 muda wote huo walikuwa hawalimi.

"Malipo yamefanyika bila kujali thamani ya shilingi kwa zaidi ya miaka mitatu, mazingira ya bahari yameharibiwa wavuvi wa pale Chongoleani kwa sasa ni kama hawana shughuli za kufanya," alisema Lenga.

Mkurugenzi Mwanzishilishi wa ECO, Richard Senkondo alisema wanaendelea kufanya juhudi za kukutana na Balozi wa China hapa nchini ili kumueleza na kumtaka kutembelea mradi huo ili kuona uharibifu wa mazingira uliofanyika.

"Mpaka Agosti 13 mwaka huu jumla ya kampuni 28 kubwa duniani na taasisi 27 za bima na mabenki zimetangaza kuupinga mradi huu baada ya kuona namna haki za binaadam zilivyopokwa na hatari za kimazingira zinazoweza kutokea kwenye maeneo linakopita bomba hilo.

"Kampuni hizo za bima na mabenki zinatoka Magharibi hii inaonesha kwamba wao wanaheshimu sana haki za binaadam sasa bado China ambayo imeonesha nia ya kuja kuwekeza kwenye mradi huo kupitia kampuni yake kubwa ya bima.

"Naamini wangetembelea maeneo ya mradi wasingekubali kuwekeza... ndio maana tunapambana kabla hawajaingiza fedha zao huko waje tukawaoneshe hili tunalowaeleza," alisema Senkondo.

Alisisitiza kwamba wanaziomba Serikali za Uganda, Tanzania na Kampuni ya Total Energies warudi mezani kuona athari za kimazingira zitakazotokea miaka michache ijayo iwapo watatekeleza mradi huo.

Kwa mujibu wa Senkondo mradi wa EACOP uuliotarajiwa kugharimu dola bilioni tano za Marekani humu ukitarajiwa kukamilika mwaka 2025 mpaka sasa Agosti, 2024 umetekelezwa kwa asilimia 40 tu.

Alisema maradi huo unachukua asilimia 80 ya eneo la utekelezaji huku Uganda wakitumia asilimia 20 ya eneo lao kwenye mradi huu.

Senkondo alishauri ufanyike upembuzi huru utakaohusisha wataalam kutoka nje ya nchi ili kuona athari za kimazingira kwenye maeneo ya mradi huo na baharini, lengo ni kuona namna ya kupunguza ama kuondoa kabisa hofu ya uharibifu wa mazingira na ekolojia huku taifa likikabiliana na mabadiliko hasi ya tabianchi.

Mratibu wa EACOP, Asiad Mrutu amekiri kuwepo kwa kampeni ya muda mrefu kuzuia utekelezaji wa bomba hilo la mafuta ghafi.

"Zipo kampuni zilizojitoa lakini sio suala la kutolea ufafanuzi kwenye simu, nakukaribisha ofisini ndugu mwandishi tuzungumzie hilo," alisisitiza.

Juhudi za kumpata msemaji wa suala hili kwenye ubalozi wa China zinaendelea.
Mwakilishi wa Shirika la Green Faith, Baraka Lenga kulia akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuupinga EACOP kushoto ni Mkurugenzi Mwanzishilishi wa Taasisi Organization for Community Engagement, Richard Senkondo.

Post a Comment

0 Comments