Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika leo Septemba 20,2024 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,(hayupo pichani ) wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika leo Septemba 20,2024 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq,akizungumza wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika leo Septemba 20,2024 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe,akizungumza wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika leo Septemba 20,2024 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika leo Septemba 20,2024 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Na WMJJWM, Kilimanjaro
Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii inayojitegemea chini ya Wizara yenye dhamana ya masuala ya Ustawi wa Jamii ili kurahisisha na kuimarisha uratibu, usimamizi na utekelezaji wa afua za Ustawi wa Jamii nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima Septemba 20, 2024 wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri Dkt. Gwajima amesema lengo la kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii itakayojitegemea ni ongezeko la uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii kisekta kunakohitaji Taasisi madhubuti katika kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hizo katika jamii kupitia Taasisi za umma, binafsi na wananchi kwa ujumla.
Amebainisha kwamba, hatua hiyo ni matokeo ya kukubaliwa kwa wasilisho la mapendekezo ya Haki Jinai kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo mpango huo kwa sasa unasubiri maelekezo ya muundo wa Idara hiyo kupitia Wizara ya Utumishi.
"Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii namba moja kwa kutambua mchango wa kazi zenu na kuipa kipaumbele tasnia hata kubariki tuendelee kufanya mkutano huu kila mwaka ili kupata nafasi ya kujifunza mambo mazuri kutoka kwa wenzetu na kujadili namna ya kutatua changamoto za ukatili wa aina mbalimbali zinazoikumba jamii yetu kwa sasa pamoja na namna ya kuboresha mazingira ya kazi tunapotekeleza majukumu yetu."amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amesema elimu itakayotolewa na Maafisa hao itasaidia jamii kuelewa mambo mbalimbali ya huduma za kiustawi hasa huduma za unasihi kwa watoto, wazazi/walezi, huduma za uchangamshi wa awali ya watoto wadogo na huduma ya Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia na kijamii kwa makundi yenye uhitaji.
Aidha, amesema Familia ndio taasisi pekee ambayo ni nguzo muhimu katika malezi bora inayomuandaa mtoto kuwa mwanaume au mwanamke bora wa baadaye na familia ndiyo mahali salama kwa watoto kukua na kufikia utimilifu wao hatimaye kuwa raia wema, wenye maadili na wazalendo watakaochangia ustawi waTaifa letu hivyo ni lazima kuwekeza katika kutoa elimu ya umuhimu wa familia kwa wazazi na walezi.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba, familia zimekuwa zikikukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo umaskini, migogoro ya ndoa na familia, malezi duni kwa watoto inayopelekea kukosekana kwa muunganiko na mahusiano hafifu kati ya wazazi au walezi na watoto wao, ambapo athari zake ni pamoja na watoto kukosa upendo wa wazazi au walezi.
Ameeleza kuwa kuendelea kuwepo kwa mila na desturi za kukaa kimya na kuficha taarifa za vitendo vya ukatili hasa vinavyotokea ndani ya familia imesababisha kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili na kukosekana huduma kwa wahanga hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili na tabia hatarishi kwa watoto.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amewapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii kwa msisitizo wana mchango mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq,amesema, anatambua kuwa Wataalam hao wamefanya tathimini ya mambo yote yanayotakiwa ili kuboresha utendaji kazi zao na kutatua changamoto zao, ambapo Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kuongeza Bajeti ili kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wenye kaulimbiu Tanzania Bila Ukatili Inawezekana, Imarisha Mahusiano Ndani ya Familia”, umefanyika kwa muda wa siku tatu, Septemba 18 – 20, 2024 Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
0 Comments