Ticker

6/recent/ticker-posts

MHE. KATAMBI AKEMEA VIKALI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WENYE UALBINO

Na; Mwandishi Wetu – DODOMA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amekemea vikali vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya Watu wenye Ualbino na kueleza kuwa wanaofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Kumekuwa na changamoto juu ya makundi maalum ya Watu wenye Ulemavu, Wanawake na Watoto, hivyo katika kukabiliana na changamoto hizo serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha inaondoa changamoto hizo,” amsema.

Mhe. Katambi amebainisha hayo leo Septemba 21, 2024 wakati wa kongamano la Binti mwenye Ndoto, lililolenga kupinga ukatili, mauaji ya watoto, wanawake na unyanyapaa dhidi ya Watu wenye Ualbino kuelekea kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani linalofanyika jijini Dodoma.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kuelimisha jamii kuhusu haki za Watu wenye Ulemavu sambamba na kupambana na unyanyasaji, ramli chonganishi, mila potofu na mauaji ya Watu wenye Ualbino.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda ametoa rai kwa jamii kuendelea kupinga vitendo vya kikatili wanavvyofanyiwa Watu wenye Ulemavu, hivyo amewasii pindi wanapoona matukio hayo watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Cde. Rehema Sombi ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu nchini wakiwemo wenye Ualbino ili kuhakikisha kundi hilo linapata haki zao za msingi.

Akizungumza awali Mkurugenzi wa Asasi ya Watu Wote ni Sawa (WAWOSA), Magreth Swai amesema watu wenye Ualbino wanahaki kama watu wengine, hivyo ametaka jamii kuendelea kuwalinda, kuwathamini na kuwashirikisha katika shughuli za kijamii.

Kongamano hilo lilijikita katika uwezeshaji mabinti katika Nyanja mbalimbali kama vile masuala ya Uongozi, Teknolojia, Biashara na uwekezaji, Malezi na mahusiano ya kijamii, Ubunifu wa Mavazi na Kilimo ambapo limeongozwa na kauli mbiu isemayo “Ualbino siyo laana wala mikosi, Mlinde, Mthamini, Mshirikishe katika shughuli za kijamii,”


Post a Comment

0 Comments