Ticker

6/recent/ticker-posts

Mashirikiano PURA, ZPRA yazidi kuimarika

Mashirikiano kati ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara na Mamlaka ya Uthibiti, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Zanzibar (ZPRA) ya Zanzibar yameendelea kuimarika kufuatia jitihada za dhati zinazofanywa na uongozi wa Taasisi hizo kutekeleza Hati ya Makubaliano waliyoingia mwaka 2022.

Hayo yamedhihirika wakati wa kikao cha menejimenti za PURA na ZPRA kilichofanyika Septemba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili taarifa ya utekelezaji wa mashirikiano baina ya Taasisi hizo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ZPRA, Mha. Mohammed Slum Said, wajumbe wa menejimenti wa Taasisi hizo na wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Ufundi (Joint Technical Committee - JTC) iliyoundwa kuwezesha utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano iliyowasilishwa na JTC, kwa mwaka 2023/24 PURA na ZPRA zilishirikiana katika maeneo mbalimbali yakiwemo durusu ya mikataba kifani ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato, maandalizi ya miongozo ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR Guidelines), mafunzo ya kaguzi za mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato (PSA audits) na uhifadhi wa data za petroli.

Maeneo mengine ni maandalizi ya mkakati wa kunadi vitalu, uzinduzi wa duru ya kwanza ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Zanzibar na utangazaji wa vitalu hivyo kupitia mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki kikao cha menejimenti ya PURA na ZPRA kilichofanyika Septemba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa mashirikiano kati ya taasisi hizo kwa mwaka 2023/24.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni (kulia) akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao cha menejimenti za PURA na ZPRA kilichofanyika Septemba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mashirikiano baina ya taasisi hizo kwa mwaka 2023/24. Kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPRA, Mha.  Mohammed Slum
Sehemu ya wajumbe walioshiriki kikao cha menejimenti ya PURA na ZPRA kilichofanyika Septemba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa mashirikiano kati ya taasisi hizo kwa mwaka 2023/24

Post a Comment

0 Comments