Na Hamida Kamchalla, MOROGORO.
JAMII imehamasishwa kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani na kutembelea vivutio vilivyopo katika maeneo yao kwani vitasaidia kuwajengea taswira pana ya nchi na kuwa mabalozi kwa raia wa kigeni.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala kwa upande wake amewahimiza wananchi wilayani humo na maeneo ya jirani kutembelea kivutio cha chemichemi ya maji moto kilichopo katika kata ya Kisaki, halmashauri ya Morogoro vijijini.
Kilakala ametoa hamasa hiyo alipotembelea kijijini hapo na kujionea kivutio cha chemichemi inayotoja maji ya moto muda wote na siku zote bila kikomo wala kupoa kwa maji hayo hata ikinyesha mvua.
"Mwenyezi Mungu ametubariki katika maeneo yetu, tunayo chemichemi ya maji moto, muda na wakati wote, iwe kipindi cha jua au mvua maji yanakuwa ya moto, hususani majira ya asubuhi maji haya yanatoka mvuke, karibu wilayani kwetu katika Kijiji hiki mjionee maajabu haya makubwa" amehimiza.
Naye Afisa Mali Asili Wilaya ya Morogoro Wahida Beleko amesema chemichemi za maji moto zipo pia katika baadhi ya hifadhi nchini lakini yanatofautiana ikilinganishwa kiwango cha joto kilichopo.
"Chemichemi hizi zipo maeneo mengi, yapo hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, hata Ziwa Manyara yapo lakini ya kwetu kidogo ni tofauti, haya joto lake ni kali sana hasa majira ya asubuhi,
"Cha ajabu hata mvua ikinyesha tunatarajia kuwa yatapozwa kutokana na maji ya baridi, lakini ndiyo yanakuwa yamoto zaidi, na maji haya kitaalamu yanatibu magonjwa ya ngozi" amesema.
0 Comments